Na Khamis Haji , OMKR
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka
wanachama na viongozi wa chama hicho wasivunjike moyo na matokeo ya
uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiembesamaki na badala yake waendelee na
juhudi za kukiimarisha chama, ili kiweze kukamata dola katika uchaguzi
mkuu wa mwakani.Akifungua
mkutano wa viongozi wa matawi, majimbo na Wilaya kwa Wilaya za Wete na
Micheweni uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete,
Maalim Seif amesema kilichotangazwa Kiembesamaki si matakwa ya wananchi,
kwa vile kimsingi wananchi wa jimbo hilo walisusia uchaguzi huo.
Maalim
Seif amesema idadi kubwa ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi
huo si wakaazi wa eneo hilo, ambao walichukuliwa katika maeneo mbali
mbali, baada ya kubainika wananchi wenyewe hawatashiriki kwa sababu
hawakuridhishwa na maamuzi yaliyochukuliwa hadi kufanyika uchaguzi huo.
“Kama
kuna wananchi wa Kiembesamaki waliokwenda kupiga kura basi hawazidi
1000, wengi walichukuliwa katika maeneo tafauti, kama vile Makunduchi,
Mtende, Kitope na Bumbwini na wakapelekwa kupiga kura huku wakilindwa na
vikosi vya Serikali”, alisema Maalim Seif.
Amesema
mbali na hayo kuna baadhi ya wananchi wa Kiembesamaki walipewa vitisho
kabla ya kufanyika uchaguzi huo, kwa kutumiwa ujumbe unaowaonya
wasijitokeze kwenda kupiga kura, vyenginevyo watapatwa na matatizo
makubwa.
Katika
uchaguzi huo mdogo wa Kiembesamaki ambao uliofanyika Februari 2, mwaka
huu, baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, Mansour Yussuf Himid
kutimuliwa uanachama wa CCM, mgombea wa CCM, Mahmoud Thabit Kombo
alitangazwa mshindi, ambapo vile vile idadi kubwa ya wapiga kura
hawakujitokeza kwenda kupiga kura.
Akizungumzia
Katiba Mpya, Maalim Seif amewahimiza wajumbe wa Bunge la Katiba kuweka
kando maslahi ya vyama au makundi yao, na badala yake wahakikishe
Tanzania inakuwa na Muungano wa haki, ambapo Wazanzibari na Watanganyika
kila upande uridhike kuwa unapata haki sawa na mwengine.
“Kwa
upande wetu Wazanzibari tusisahau tuna kilio kikubwa cha miaka mingi
kutotendewa haki ndani ya Muungano huu, wajumbe wote wajali maslahi ya
Zanzibar na waweke pembeni maslahi binafsi au ya vyama vyao”, alionya
Maalim Seif.
Kuhusu
uchaguzi mkuu unaoendelea ndani ya CUF, Katibu Mkuu huyo amesema kwa
wale viongozi ambao tayari wamechaguliwa katika ngazi za matawi na
Majimbo wajiepushe na tabia ya kuwatenga wale ambao hawakushinda, na
wafanyekazi kwa pamoja kwa ajili ya kukiimarisha zaidi chama.
Amesema
kitendo cha kuwatenga walioshindwa katika shughuli za kichama itakuwa
ni dhambi kubwa ambayo itasababisha mifarakano na kupelekea hata hao
walioshinda wasiweze kufanya kazi kwa ufanisi na matokeo yake ni
kudhorota ufanisi katika utekelezaji wa malengo ya chama.
No comments:
Post a Comment