WATU
wawili wa familia moja wameuawa wilayani Maswa mkoani Simiyu, kwa
kupigwa na wananchi waliojichukulia sheria mikononi, wakiwatuhumu kuzuia
mvua kunyesha hivyo kusababisha ukame kwenye eneo lao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alitaja waliouawa ni Gilya Chile (70) na mjukuu wake, Nyangu Nyambalya (30).
Polisi
inashikilia watu wanane akiwemo Kamanda wa Sungusungu, Sosoma Masamuda
(50), Ligwa Malimi wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Wengine
ni Emanuel Kasmiri (42), Michael Sospeter (18), Toto Emanuel (28),
Nyanzobe Ntinga (26) Tabu Zengo (31) na Joyce Kija (30). Baada ya
uchunguzi wa polisi kukamilika, watafikishwa mahakamani kujibu
mashitaka.
Mauaji hayo yalifanyika usiku wa kuamkia juzi katika kijiji hicho, Kata ya Mwanhonoli wilayani Maswa.
Inadaiwa
sungusungu wa kijiji hicho waliitana usiku na kuafikia katika kikao
chao kwenda kuwaamsha babu na mjukuu wake waeleze sababu za kuzuia mvua
kunyesha.
"Usiku
huo walinzi hao wa jadi waliwakamata watuhumiwa hao waliokuwa wamelala
nyumba tofauti wakawahoji kwa nyakati na maeneo tofauti na kuwataka
watoe maelezo ya kutosha ya sababu ya wao kuzuia mvua isinyeshe mpaka
mazao kuanza kukauka katika mashamba ya wakulima wa kijiji hicho,’’
alisema kamanda.
Inadaiwa
sungusungu hawakuridhishwa na maelezo ndipo walianza kuwasulubu kwa
kipigo na kuwasababishia mauti kabla ya kuteketeza miili yao.
Kamanda
alisema, uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kabla ya vifo vyao,
watuhumiwa walikuwa wakitamba kwenye vilabu vya pombe kuwa wanatoka
kwenye familia ya kitemi hivyo wana uwezo wa kuleta mvua au kuizuia
isinyeshe.
Kwa
mujibu wa kamanda, tambo hizo zilifanyika kipindi ambacho kijiji hicho
kilikumbwa na ukame. Inadaiwa watu hao walishauri wananchi wa kijiji
hicho wawachangie gunia moja la mahindi au mtama kila kaya walete mvua.
Chanzo;Habari Leo
No comments:
Post a Comment