Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, February 25, 2014

WAZIRI NYALANDU AWANG'OA VIGOGO IDARA YA WANYAMAPORI AKIWEMO MKURUGENZI WA WANYAMA PORI.

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu leo ametangaza kuwang'oa
vigogo wa ngazi ya juu katika Idara ya wanyamapori akieleza kuwa ni
kutokana na kutoridhishwa na utendaji wao. 

Ifuatayo ni Taarifa rasmi ya tamko la Waziri Nyalndu,  kama alivyolisoma leo:

Leo, TAREHE 24 Februari, 2014 Natangaza kuubadili uongozi wa Idara ya 
Wanyamapori ya Wizara ya maliasili na Utalii kama ifuatavyo:  Ninamuondoa Profesa Alexander Songorwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii.  
Nachukua hatua hii kutokana na kutokuridhishwa kwangu na utendaji wa kazi wa idara hiyo katika
mapambano dhidi ya ujangili yanayoendelea nchini.
Aidha, hatua hii ni utekelezaji wa 
Azimio la Bunge lililotolewa tarehe 22 Disemba, 2013, lililotaka 
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za 
uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza.  
Utekelezaji wa agizo hili unaanza mara moja, nami namteua Bwana Paul 
Sarakilya kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya 
Wziara ya Maliasili na Utalii kuanzia sasa. 
Aidha, ninamuondoka Profesa Jafari 
Kidegesho katika nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya 
Wanyamapori na kumteua Dr. Charles Mulokozi kuchukua nafasi hiyo.  Hali 
kadhalika, ninamteua Bwana Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi 
Uzuiaji – Ujangili na anachukua nafasi ya anayeenda kuwa Kaimu 
Mkurugenzi wa Wanyamapori. 
Vilevile, Bibi Nebbo Mwina 
anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu, na 
Bwana Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji
wa Wanyamapori. Pamoja na Kitengo cha Uzuiaji – Ujangili nilichokitaja 
awali, hivi ni vitengo vya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya 
Maliasili na Utafiti. 
Nawaagiza kwamba Wakurugenzi na 
Wakuu wote wa kila Idara, kila Shirika, na Taasisi zote ndani ya Wizara 
ya Maliasili na Utalii kutengeneza viashiria muhimu vya utendaji kazi 
(Key Performance Indicators) na kukabidhi kwangu ndani ya siku 30 
zijazo.  
Viashiria hivi ni hatua ya 
kufanikisha yafuatavyo, 1)  Malengo ya wizara, 2)  Uwajibikaji, 3) 
Uwazina 4) Ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku.  Ni sharti 
tutekeleze mikakati ya wizara katika mifumo inayopimika, tuweze kujipima 
natuweze kupimwa, natutumikie Taifa kwa uadilifu. 
Kwa mtumishi wa Wizara ya Maliasili  
na Utalii ikiwemo mimi mwenyewe, Lazaro Nyalandu, atapaswa kuzingatia na 
kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Mwenendo (Code of 
Conduct) ambazo zitapendekezwa na kupitishwa na Baraza la Wafanyakazi wa 
Wizara. 
 Baraza hili liwe limeitishwa na 
Katibu Mkuu wa Wizara kabla ya mwisho ya mwezi ujao.  Azma ya kanuni 
hizi ni kuwa na misingi bora ya utumishi, uwajibikaji, utu, usawa na 
haki katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.


 Mungu ibariki Tanzania.
Asante.
 Lazaro S. Nyalandu (MB)
Wizara ya Maliasili na Utalii
24/02/2014

No comments:

Post a Comment