Pages

Saturday, February 22, 2014

Wengi hawana imani na Bunge la Katiba




WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam wameiambia Raia Mwema kwamba hawana imani na Bunge Maalumu la Katiba lililoanza kazi jana Jumanne mjini Dodoma.


Maoni hayo yamo katika utafiti uliofanywa mwishoni mwa Januari na mwanzoni mwa Februari mwaka huu (2014), chini ya mradi ambao unashirikisha Raia Mwema, taasisi ya Centre for Economic Prosperity na DataVision.

 
Utafiti wa aina hii ulikuwa ukifanywa na taasisi ya Uwezo/Twaweza. Sasa utakuwa ukifanywa na kuchapishwa chini ya mwavuli wa Raia Mwema.


Katika sehemu ya matokeo ya utafiti huo, wakazi wengi wa Wilaya zote tatu za Dar es Salaam waliohojiwa kwa njia ya simu za mkononi walionyesha kutokuwa na imani na Bunge la Katiba.


Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa asilimia 42 wana imani ndogo na Bunge Maalumu la Katiba, na asilimia 11 hawana imani kabisa Bunge Maalumu la Katiba. Asilimia 29 walisema wana imani na Bunge hilo.


Aidha, pamoja na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia wingi wao kupitisha hoja ya kusitishwa kwa kazi za Tume ya Marekebisho ya Katiba, wananchi wengi waliohojiwa walitaka Tume hiyo iendelee kuwapo.


Hoja ya Tume hiyo kubaki hai ililigawanya Bunge katika makundi ya CCM na Upinzani na matarajio ya wengi ni kwamba hali hiyo ya mgawanyiko itajirudia katika kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kilichoanza jana mjini Dodoma.


Kama ilivyo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, CCM ina wabunge wengi pia katika Bunge Maalumu la Katiba, idadi ambayo inawapa nafasi kufanya maamuzi yoyote kama ilivyofanya kupitisha kutoendelea kwa kazi za Tume ya Marekebisho ya Katiba.


Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 43 walitaka Tume ibaki; asilimia 40 walitaka isibaki, asilimia 15 hawakuonyesha msimamo wowote na asilimia mbili walikuwa hawajui chochote kuhusu jambo hilo.
RAIA MWEMA

No comments:

Post a Comment