WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye
Mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika timu ya Yanga imeingia kambini
katika hotel ya Laico Ledger iliyopo eneo la Bahari Bahari Beach
Kunduchi kujiandaa na mchezo wa siku ya Jumamosi dhidi ya timu ya Al
Ahly kutoka Misri.
Mchezo huo wa Yanga dhidi ya Al Ahly utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Ofisa Habari wa Yanga Baraka Kizuguto alisema kikosi cha Yanga chenye
wachezaji 25 pamoja na benchi la Ufundi kilianza mazoezi juzi jioni
katika Uwanja wa Kaunda Makao Makuu ya Klabu na jana asubuhi kimeendelea
kujinoa katika Uwanja wa Boko Beach.
“Wachezaji wote wapo katika hali nzuri, mpaka sasa hakuna mchezaji majeruhi kuelekea mchezo huo,”alisema
Alisema Kocha anatambua mchezo huo utakua
ni mgumu, kwani Al Ahly wana uzoefu na michezo ya kimataifa lakini na
wao wana malengo na zaidi ni kufanya mapinduzi kwa kushinda
“Kwa vile Kocha anawafahamu Al Ahly vizuri
hakuna kitakachoshindikana kwasababu tayari tumepata mbinu zao kutoka
kwa Kocha Msaidizi Boniface Mkwasa, kilichobaki ni kuwaandaa wachezaji
kiakili,”alisema.
Katika mchezo huo, Mshambuliaji wa
Kimataifa Emanuel Okwi atakuwa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika
kikosi kitakachotua dimbani siku hiyo. Kizuguto alithibitisha ushiriki
huo kwa kuonyesha leseni yake iliyotoka Shirikisho la Soka Afrika(CAF) .
Al Ahly imewasili leo alfajiri saa 12
kasorobo kwa Shirika la Ndege la Misri Egypt Air kikiwa na watu 35
wakiwemo wachezaji 22, bechi la Ufundi 8 pamoja na viongozi 5 na
wamefikia katika Hotel ya Hyatt Kempsinki ambapo ndio itakuwa ikiweka
kambi.
Siku ya Jumatano na Alhamisi jioni
watafanya mazoezi katika Uwanja wa IST uliopo Upanga, na Ijumaa jioni
watapata fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi.
Tiketi zitauzwa kwenye vituo mbalimbali
kuanzia Ijumaa ambapo kiingilio cha juu ni Shs 35,000, 25,000, 13,000
na cha chini kwa viti vya kijani na bluu ni Sh. 7000.
Rekodi ya Al Ahly:
Wana mataji 19 moja zaidi ya mataji 18 ya Ac Milan
Imeshinda mara 8 kombe la mabingwa barani
Afrika, mwaka 1982,1987,2001,2005,2006, 2008, 2012, na 2013. Makombe 4
ni ubingwa wa Kombe la washindi 1984,1985,1986, 1993.
Mara sita imetwaa kombe la CAF Super Cup 2002, 2006,2007,2009, 2013, na 2014 na mmoja likiwa la Afro-Asian Cup mwaka 1988.
No comments:
Post a Comment