Pages

Tuesday, February 18, 2014

ZIARA YA NAIBU WAZIRI WA MAJI MKOANI MOROGORO YAMALIZIKA



Naibu Waziri, Amos Makalla akiwa katika mradi wa maji, kijiji cha Lupiro. 
Kituo cha kusukumia maji na tanki la kuhifadhi maji katika mradi wa maji, kijiji cha Lupiro. Tanki la kuhifadhi maji, mradi wa maji wa kijiji cha Lupiro.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, (kushoto) pamoja na viongozi na watendaji wengine wa Serikali katika mradi wa maji wa Ulanga mjini.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiangalia chanzo cha maji cha Kibulubutu, wilaya ya Kilombero.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akiwa katika mkutano na viongozi na watendaji wa Serikali katika wilaya ya Kilombero.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akipokea zawadi ya kifaa cha kuchujia maji kwa ajili ya kupata maji safi na salama ya kunywa kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya MSABI ya wilaya ya Kilombero, Dale Young.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla amemaliza ziara yake ya siku tisa mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki
Mhe. Makalla amemaliza ziara hiyo kwa kutembelea miradi ya maji ya Halmashauri za Wilaya za Ulanga na Kilombero na kukagua utekelezaji wake.
"Utekelezaji unaenda vizuri, isipokuwa kasi iongezwe ili miradi yote ikamilike kwa wakati, na nitafuatilia kwa ukaribu miradi yote niliyoikagua na nitarudi kuangalia maendeleo yake". Wakati umefika kuhakikisha sekta ya maji inatekeleza sera zake ipasavyo na kuachana na masuala ya siasa kama wananchi walivyozoea na kusababisha kukosa imani na Serikali yao", alisema Mhe. Makalla.
Naibu Waziri aliendelea kwa kusema Serikali imetenga pesa za kutosha kukamilisha miradi hii, kwa hiyo, hakuna sababu nyingine yoyote ya kutokamilisha miradi hii. Nataka nisikie wakandarasi wamekamilisha miradi hii na wanadai pesa za malipo na sio wanadai wakati kazi hazifanyiki. Ninachosisitiza ni ufuatiliaji wa karibu kwa watendaji wote wa Serikali na kuhakikisha kazi inafanyika vizuri bila visingizio vyovyote.
"Nimeahidiwa kuwa mradi wa kijiji cha Lupiro utakuwa umekamilika ifikapo tarehe 01/03/2014. Hivyo, nategemea kuja kuufungua rasmi siku hiyo ili wakazi wa hapa na jirani zake waanze kupata maji safi na salama", aliongeza Naibu Waziri Makalla.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mji wa Morogoro (MORUWASA), Inj. Halima Mbiru alisema Serikali, Halmashauri na MORUWASA kila mmoja imetenga fedha za kutosha katika kutekeleza miradi yake yote kwa muda uliopangwa.
Akasisitiza kujituma na kufanya bidii kwa wahusika wote ili kufanikisha lengo hilo na kuondokana na tatizo la maji mkoani humo. Mhe. Makalla alitembelea kijiji cha Lupiro ambacho ni moja ya vijiji kumi, vinavyotekeleza mpango wa BRN. Pia, alifika kwenye chanzo cha maji cha Kibulubutu, wilayani Kilombero ambacho Serikali ina mpango kutumia maji yake kwa wakazi wa mji huo katika azma ya kumaliza tatizo la maji.
Hii ni ziara ya pili ya Naibu Waziri, Amos Makalla tangu aanze kazi katika Wizara ya Maji baada ya ile ya kwanza aliyoanza Dar es Salaam wiki tatu zilizopita.
CHANZO:MTAA KWA MTAA

No comments:

Post a Comment