Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, March 9, 2014

HUYU NDIO KOCHA MPYA WA TAIFA STARS "Martinus Ignatius ‘Mart"KUANZA KAZI 24 MARCH


  Jamal Emil Malinzi.
Tangu TFF kusema inatafuta kocha mpya atakayerithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen, mtandao huu umekuwa ikifuatilia kwa undani mwalimu mpya wa Stars atakuwa nani na sasa inaibuka na jibu ni Mart Nooij.
Tayari Nooij ambaye kwa sasa ni kocha wa St George ya Ethiopia amekwishasaini Mkataba wa miaka miwili na TFF na atakuja nchini mwishoni mwa mwezi huu.



Ulikuwa mchakato makini, uliohusisha wataalamu na washauri wa kimataifa juu ya masuala ya ufundi ya soka ambao umefanikisha kupatikana mwalimu huyo wa Kiholanzi aliyezaliwa Julai 3, mwaka 1954 mjini Beverwijk, Uholanzi.
Nooij amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12. 
Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya  AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kunyakuliwa na St George ya Ethiopia anakoendelea na kazi hadi sasa.
Baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili na TFF kuja kuifundisha Stars, Nooij anasubiri barua maalum ya kuruhusiwa kuondoka baada ya kukamilisha taratibu za kuvunja Mkataba uliokuwa unaelekea ukingoni na klabu hiyo ya Addis Ababa. 
Yanga SC pia inafundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm.

CHANZO: BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment