Tukiacha
mbali picha ambayo mara nyingi au kwa miaka mingi imekuwa ikijengwa
vichwani mwa wengi wanapoona na kudhani kwamba fulani ni kiongozi bora
[pengine kwa muonekano tu], au kwa sababu anashuka kutoka kwenye gari
kwa mbwembwe, tabasamu baada ya kufunguliwa mlango na mkanda na kisha
kupokelewa briefcase yake, yapo mambo kadhaa ambayo yanamfanya mtu awe
kiongozi bora na sio bora kiongozi. Na kadri siku zinavyokwenda, taswira
ya kiongozi kwa muonekano tu inazidi kupotea.
Vitendo,maadili,mafanikio, uvumbuzi na maendeleo vinachukua mstari wa
mbele.
Tofauti
na miaka ile ambayo picha ya kiongozi bora ilikuwa kama hiyo hapo juu,
siku hizi viongozi bora wapo na wanajitokeza katika hali tofauti tofauti
kabisa. Anaweza kuwa asiyevaa suti kama Dalai Lama na akawa kiongozi
bora. Au asiyevaa suti bali t-shirt na jeans tu kama alivyokuwa Steve
Jobs wa Apple au Mark Zuckerberg boss wa Facebook. Mifano ya viongozi
hawa ipo mingi.
Kituo
cha utafiti na mafunzo ya uongozi cha Dale Carnegie cha jijini New York
nchini Marekani kinasema katika utafiti wao wamegundua kwamba
kinachomfanya mtu awe kiongozi bora sio suti, briefcase, tabasamu[
hususani lile la uongo] bali uwezo na nia ya dhati katika kuamsha ari,
kuwawezesha unaowaongoza, kuwafanya wajiamini na kuwapa motisha watu
unaowaongoza.
Pamoja
na hayo, na kutokana na ukweli kwamba leo hii tuna kila aina ya
viongozi, yapo baadhi ya mambo yanayowatofautisha viongozi bora na bora
viongozi. Haya hapa ni baadhi yake;
1. Aweze Kuyakabili Matatizo au Changamoto
Kiongozi
bora ni yule ambaye ana ujasiri wa kutosha wa kukabiliana na kila aina
ya changamoto au matatizo ambayo yanaweza kujitokeza iwe aliyatarajia au
hakuyatarajia.
Dunia
ya leo imejaa changamoto za kila aina. Kila kukicha kuna jipya na gumu
zaidi. Uchumi umeporomoka, fedha haina thamani tena, kimbunga kikali
kimekuja na kuipindua juu chini shule ya kijiji. Kiongozi bora
anafanyaje? Anapotelea mjini kwa kisingizio cha kuwa “bize” au anakuwepo
bega kwa bega kutatua tatizo?
Jibu
lipo wazi. Kiongozi bora atakuwepo na kuwasiliana na kila mtu
anayemuongoza iwe ni ofisini au jimboni kuhusu ukweli halisi na ukubwa
wa tatizo na jinsi ambavyo yeye kama kiongozi analishughulikia [kwa
kushirikiana na kila mtu wakiwemo anaowaongoza] tatizo au changamoto
husika.
2.Awe Muaminifu
Kiongozi
bora lazima awe muaminifu. Uaminifu unaanzia kwenye kuwa mkweli.
Anaposema atafanya hili au lile, alifanye. Asipolifanya, awe muwazi na
kuwaeleza wale anaowaongoza ukweli wa sababu zilizofanya asitimize ahadi
yake na jitihada anazofanya kutimiza ahadi yake.
Kwa
mfano wananchi wanapomchangua “kiongozi” kutokana na sera na ahadi za
kutatua tatizo la ukosefu wa maji safi jimboni kwao kisha miaka mitano
baadae ahadi hiyo ikawa haijatimia, ni wazi kwamba imani kwa kiongozi
huyu itafifia kama sio kupotea kabisa. Mbaya zaidi pale atakapokuja na
sababu ambazo hazina mashiko huku kila mtu akiona wazi kwamba ahadi yake
ilikuwa ahadi hewa au ya kisiasa.
Onyesha
kwamba unawajali na kuwathamini unaowaongoza. Yaelewe matatizo na
changamoto za unaowaongoza. Shirikiana nao bega kwa bega kuyatatua.
Usiwe kiongozi wa ofisini tu bali nenda kule walipo. Na usiende kwa nia
ya kupigwa picha tu. Ili wakuamini ni muhimu wakaona kwamba wewe sio
“mwizi” tu wa fursa.
3. Kuwa Halisi [Asiwe Feki]
Mojawapo
ya mambo ambayo sio tu yanamfanya mtu awe bora kiongozi bali apoteze
kabisa hata nafasi ya kuongoza ni pamoja na kuwa “feki”. Ni rahisi sana
kwa mtu/watu kutambua kwamba huyu si yeye. Anajifanya kuwa mtu ambaye
siye.
Kwa
bahati mbaya hakuna mtu anayependa “feki”. Viongozi wanasiasa huanguka
sana kwenye mtego huu. Wengi wanadhani wananchi hupenda kusikia mashairi
na ngonjera tamu tamu pekee. La. Labda zamani. Siku hizi ukiwa
kitimbakwila utajulikana kirahisi na utakuwa nje ya ulingo. Wenzetu
wanasema Walk The Walk and Talk The Talk.
Hata
kama wewe ni kiongozi wa ofisi au mfanyabiashara, pindi tu utakapokuwa
“feki” wateja wako watajua. Watakukimbia. Watahisi hata vitu unavyouza
ni “feki” kwa sababu wewe mwenyewe unaonekana feki au unajibeduisha kuwa
sivyo. Kuwa orijino. Unapenda kucheka au kuchekesha? Cheka. Wachekeshe
unaowaongoza. Unapenda muziki? Usihofu kuonyesha wazi kwamba unapenda
muziki. Tumia vitu unavyovipenda au maarifa unayoyamudu zaidi
kutengeneza aina yako ya uongozi.
4.Ajiheshimu
Kiongozi
bora lazima ajiheshimu. Na dhana ya kujiheshimu ni pana. Kuna
kujiheshimu katika nyumba na mahusiano yako iwe na wanao, mkeo, wazazi
wako, ndugu, jamaa na hata marafiki. Kuna kuiheshimu ofisi yako na watu
unaowaongoza. Kiongozi ambaye kila siku anakabiliwa na tuhuma za ulaji
rushwa, uongo, umalaya ni wazi kwamba hajiheshimu na hivyo ni ngumu
kuwafanya watu wengine wamheshimu. Nawajua baadhi ya “bora viongozi”
ambao wametumbukia huko kutokana na tabia zao za ufuska ambazo ingawa
wanahisi watu hawajui, kwa kiasi kikubwa zimewapotezea heshima ya
uongozi na hususani uongozi bora.
Unapojiheshimu,
inakuwa rahisi kuongoza wengine. Hakuna mtu anayependa kujishirikisha
na mtu asiyejiheshimu. Watu hujisikia faraja kuhusiana au kufanya
biashara na watu wanaojiheshimu. Pia hata kama unaongoza ofisi au
biashara tu,wateja wenye akili timamu wanataka kutumia hela zao mahali
ambapo ofisi au biashara inaheshimu na kutimiza ahadi zao kufuatana na
misingi. Ukisema kwamba ninyi ndio duka lenye bei chee zaidi na bidhaa
halisi, basi iwe ni kweli. Vinginevyo inaashiria kwamba hamjiheshimu. Ni
waongo. Uongo ni sehemu ya kutojiheshimu.
5.Jifunze/ Taka Kujua Zaidi/ Nenda Na Wakati
Kiongozi bora ni yule ambaye anataka kujifunza zaidi na ni mtafiti. Mwisho wa darasa sio mwisho wa kujifunza kwa kiongozi bora. Zitto Kabwe, Mbunge
wa Kigoma Kaskazini aliwahi kunieleza katika mahojiano yangu naye jinsi
ambavyo alishangaa wakati fulani kusafiri na viongozi fulani kutoka
Tanzania mpaka Ujerumani na asione wakisoma hata vipeperushi vinavyokuwa
kwenye viti achilia mbali vitabu,magazeti nk.Viongozi bora wanauliza
maswali. Wanauliza maswali kwa nia ya kujifunza, kupata maarifa na
taarifa. Ni wasikivu na wapo tayari kufundishwa.
Kwa
bahati nzuri dunia ya leo ina kila nafasi na uwezekano wa kujifunza.
Hizi ni zama za sayansi na tekinolojia. Kiongozi bora atataka
kujua…hicho kitu kinachoitwa Twitter ni nini? Kinafanyaje kazi?
Atajiunga. Atataka kujua jinsi watu wanavyowasiliana siku hizi. Atataka
kujua jinsi nchi za wenzetu wanavyofanikiwa katika masuala mbalimbali.
Atajitahidi na kuchunguza mpaka mwisho kuona kama sayansi hiyo au
maarifa hayo yanaweza pia kutumika nchini kwake,jimboni kwake, ofisini
kwake nk. Kiongozi bora atasoma vitabu,majarida,magazeti, nk kwa nia ya
kujifunza zaidi.
6.Kuwa Mtendaji
Yote
niliyoyataja hapo juu yanakamilishwa au kuhusishwa moja kwa moja na
utendaji. Kiongozi bora haishii kwenye kuongea tu huku akijizungusha
kwenye kiti na kuagiza chai. La.Anatenda. Ananyanyuka, kwenda na kutenda
kama mfano. Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere kama kiongozi bora aliyewahi
kutokea ni kwa sababu alikuwa mtendaji. Aliongea,kuelekeza,kuonya
lakini mwisho wa siku alikuwa mtendaji.
Nyanyuka na enenda ukaifanye kazi. Onyesho kwa vitendo kwamba wewe ni kiongozi bora na sio bora kiongozi.
BOFYA HAPA LIKE PAGE YETU KWA MAKALA NYINGI
BOFYA HAPA LIKE PAGE YETU KWA MAKALA NYINGI
No comments:
Post a Comment