Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Juma Nkamia
VITISHO
vya watendaji wa serikali kwa vyombo vya habari vimezidi kushika kasi,
safari hii Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Juma Nkamia,
akitishia kuvifungia au kuvifuta.
Nkamia amebainisha kuwa magazeti yanayowachafua watu, serikali na kuhatarisha usalama wa nchi yatakumbana na kifungo.
Itakumbukwa mwaka jana serikali ililifungia gazeti la Mtanzania kwa
miezi mitatu na Mwananchi kwa wiki mbili, kwa madai ya kuandika habari
za kichochezi.
Nkamia, alitoa vitisho hivyo jana jijini hapa kwenye tamasha la
vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Voice of Youth (VOYC) lililokuwa
likijadili masuala mbalimbali yahusuyo vijana.
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakijadiliwa ni ujira, uzalendo, ujasiriamali na ajira,
Nkamia alisema hatakubali siku moja asutwe kwa kutotimiza wajibu wake katika wizara anayoisimamia, kwa kuwaachia waandishi wasiofuata maadili ya taaluma yao.
“Mimi sitaki kufanya kazi na waaandishi wa habari makanjanja, ambao
si makini na wanaofanya kazi kwa masilahi ya kundi fulani la watu.
“Tutakifuta, kukifungia chombo chochote cha habari pamoja na
waandishi wake wanaokwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari,
sitaruhusu wanaoendekeza kuwachafua wengine, umbea,” alisema.
Alisema amefanya kazi hiyo kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo
kabla ya kuingia kwenye siasa ambako sasa anasimamia wizara
inayoshughulika na waandishi wa habari.
Nkamia pia alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana waache kushiriki
kwenye maandamano yanayoitishwa na vyama vya siasa alivyoviita havina
malengo mema kwa taifa.
Alibainisha kuwa vijana hawawezi kupatiwa fedha kama hawafanyi kazi
yoyote, kwani hata mataifa yaliyoendelea ambayo ni Marekani na Uingereza
hawafanyi hivyo.
Hata hivyo katika mkutano huo, viongozi wa halmashauri na mkoa
walikacha kuhudhuria na hawakutuma wawakilishi katika tamasha hilo licha
ya kualikwa.
Kukacha kwao huko kulisababisha gumzo kubwa na Afisa Tarafa ya
Nyamagana, Maximilian Kailanga, alibeba jukumu la kumkaribisha Nkamia.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment