Pages

Monday, March 31, 2014

Rais Kikwete astushwa na ajali kubwa iliyotokea Jumamosi, Machi 29, 2014 na kusababisha vifo vya watu 21 na majeruhi 11



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amestushwa na kuhuzunishwa na ajali kubwa iliyotokea usiku wa Jumamosi, Machi 29, 2014, katika Mkoa wa Pwani ikihusisha magari matano na kusababisha vifo vya watu 21 na majeruhi 11.
Rais Kikwete amevielezea vifo hivyo kuwa siyo vya lazima na ni upotevu wa bure wa maisha ya Watanzania.
Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza, Rais Kikwete amesema: “Nimeshtushwa na kusikitishwa na taarifa ya ajali iliyohusisha magari matano na iliyotokea jana usiku katika Kijiji cha Kibupa, kilichoko kati ya Ikwiriri na Kibiti, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani, ambako maisha ya Watanzania wenzetu 19 yamepotea na wengine 11 kujeruhiwa.”


  “Kufuatia ajali hiyo, nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Mwamtumu Bakari Mahiza salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vifo vya Watanzania wenzetu hao. Nimefadhaishwa mno na ajali hiyo ambako pia wenzetu wengine 11wameumia.”

“Aidha, kupitia kwako, nawatumia ndugu, jamaa na marafiki ambao wamepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki na niko nao katika kuomboleza upotevu huu mkubwa wa maisha ya wenzetu. Msiba wao ni msiba wangu na machungu yao ni machungu yangu. Nawaombea subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke peponi roho za marehemu.”

Rais pia amewapa pole wote walioumia katika ajali hiyo mbaya akisema: “Mkuu wa Mkoa nakuomba pia uwafikishie pole zangu nyingi wote ambao wameumia katika ajali hiyo. Nawaombea Baraka za  Mwenyezi Mungu ili wapone haraka na wapate tena nafasi ya kuendelea na shughuli za kuboresha maisha yao.”

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Machi,2014

No comments:

Post a Comment