Pages

Sunday, March 23, 2014

SHABIKI ATAKAEINGIA NA KUKU AU NJIWA UWANJA WA TAIFA KUFUNGWA MDA HUU



SHABIKI yeyote atakayeingia uwanjani na mnyama yeyote iwe kuku au njiwa atakumbana na rungu la sheria ya kufungwa jela siku 90 au faini ya Sh. 100,000.

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya mashabiki wamekuwa na kawaida ya kuingia uwanjani na ndege wakiwemo kuku au njiwa na kuwashikilia muda wote wa mchezo kitendo kinachozua usumbufu kwa mnyama.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Taasisi ya Ustawi wa Wanyama Tanzania (Taweso), Dk. Thomas Kahema alisema, mtu yeyote anayeingia na wanyama uwanjani anapaswa kuhakikisha anampatia huduma muhimu mnyama vinginevyo anashtakiwa kwa mujibu wa sheria ya wanyama ya mwaka 2008.

“Sheria ipo wazi, tukimkuta mtu wa aina hiyo anapigwa faini ya Sh. 100,000 au anaenda jela kwa muda wa miezi mitatu, hairuhusiwi kubughudhi wanyama, pale uwanjani kuna kelele na huwa wanawanyima uhuru wanyama,” alisema Kahema.

Naye Mkuu wa Vikosi vya Mbwa na Farasi wa Jeshi la Polisi Tanzania, Mrakibu Mwandamizi Dk. Eugene Emmanuel aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Huo ni ukatili wa wanyama na hairuhusiwi kuingia na mnyama yeyote uwanjani bila sababu ya msingi, nazungumza na askari wangu kuwapa agizo kumkamata yeyote atakayeingia na ndege uwanjani bila sababu ya msingi.”

Hata hivyo shabiki wa Yanga, Ally Ramadhani, ambaye amekuwa akionekana na kuku mara nyingi Uwanja wa Taifa amewahi kuliambia gazeti hili kwamba huwa anaingia na kuku huyo uwanjani kwa imani ya timu yake kupata mabao.

Aliingia na kuku mmoja Yanga ilipocheza na Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika na timu hiyo ikashinda bao 1-0.
SOURCE: MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment