Abiria hao walikuwa wanasafiri na
gari dogo aina ya Toyota Pick Up namba T 170 AKZ kwenda kuhani msiba
uliotokea katika kijiji cha Kongei kilichoko Hedaru mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kilimanjaro , Robert Boaz waliofariki ni Stella John (45), Salma
Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George,
(29), Sophia Mbike (51), Ritta Kallani (55) na Kallan Stephano (55),
Kolina Mmasa (55) na Bahati Daudi (25),
Wengine ni Farida Kiondo (24) na
Maria John (33) wote wakazi wa Kongei na kwamba miili yao imehifadhiwa
katika hospitali ya Wilaya ya Same.
Boaz aliwataja majeruhi kuwa ni
Zubeda Mrindoko (42),Mipa Chediel (29) na Zubeda Mlita (32) ambao
wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kutokana na hali zao kuwa
mbaya zaidi.
Wengine waliolazwa hospitalini Same ni Joyce Kandogwe (29), Subira Juma (22), Ramadhan Msangi (31) na Adinan Rajab (31).
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:00
usiku katika barabara kuu ya Tanga-Moshi, nje kidogo ya mji wa Hedaru,
ikihusisha magari matatu ambayo ni Fuso (T 299 ANM) ikitokea Moshi
kwenda Dar es Salaam na Scania (T 737 AKW) pamoja na tela lake namba T
776 CCN ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi, kwa mujibu wa Mkuu wa
Wilaya ya Same, Herman Kapufi.
Alisema watu hao walikuwa wamepanda
gari la Diwani wa Kata ya Hedaru (CCM), Gerald Gwena aliyekuwa
amewapakia waombolezaji hao kwenye pick-up yake ambayo iligongwa kwa
nyuma na Fuso na baadaye gari hilo kuparamiwa kwa nyuma na Scania na
kisha kusababisha vifo na majeruhi.
"Waombolezaji hawa walikuwa
wanakwenda na diwani kuifariji familia ya marehemu mzee Mwanga ambaye
mtoto wake wa kiume, Dismas Mwanga alifariki baada ya kusombwa na
mafuriko”, alisema.
Alisema Dismas mwenye miaka tisa
aliyekuwa anachunga kondoo milimani alifariki dunia juzi mchana baada ya
kusombwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha mfululizo.
Alisema hata, hivyo mpaka sasa haijafahamika iwapo mvua hizo zimesababisha vifo na hasara nyingine.
Kapufi alisema kamati yake ya ulinzi na usalama imekutana kwa dharura kujadili ajali hiyo na hatua ambazo wilaya hiyo itachukua.
Kamanda Boaz, alisema chanzo cha
ajali hiyo ni kuzimika ghafla kwa gari hilo mali ya diwani Gwena ambaye
alikimbia baada ya ajali hiyo.
"Ajali hiyo ilitokea baada ya gari
hilo kuzimika na Fuso iliyokuwa karibu kuteleza barabarani baada ya
kujaribu kusimama ili isigongane na Pick Up iliyokuwa na waombolezaji,
lakini lilivutwa na tope lililokuwa limejaa barabarani kisha kugonga
kabla ya kupinduka na kuangukia upande wa kulia wa barabara ambako
kulikuwa na lori la Scania.
Kamanda alisema watu 10 walikufa papo hapo , wawili walifia hospitalini na saba wamejeruhiwa.
Alisema juhudi za kuwasaka madereva hao wa Fuso pamoja na diwani huyo zinaendelea.
No comments:
Post a Comment