TAMKO LA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA WA KUNDI LA “TANZANIA KWANZA”
23 Machi 2014
Sisi Wajumbe Wa Bunge Maalum la Katiba tunaotoka makundi mbalimbali na pia tunaoamini katika kauli mbiu isemayo “TANZANIA KWANZA”,
tunapenda kutoa tamko rasmi la kuunga mkono hotuba aliyoitoa Mheshimiwa
Rais alipokuwa akihutubia Bunge Maalum la Katiba Tarehe 20/03/2014 kama ifuatavyo:
Kwanza,
tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete, kwa hotuba yake aliyoitoa wakati akizundua Bunge Maalum
la Katiba tarehe 20 Machi 2014. Tunaamini Rais, kama Mkuu wa Nchi,
alikuwa na haki na wajibu wa kutoa mwelekeo na maono yake kuhusu Rasimu
ya Katiba na hatua hii tuliyonayo sasa ya kuipitia Rasimu kwenye Bunge
la Katiba. Tunafarijika kwamba hotuba hiyo imepokelewa vizuri na
Watanzania wengi kwenye kila kona ya nchi yetu na wengi wao wamekuwa
wakitutumia ujumbe wakituhimiza kuizingatia hotuba hiyo katika kutimiza
wajibu wetu.
Pili,
tunamshukuru Rais kwa uchambuzi wake wa kina wa Rasimu na ushauri wake
kwetu kuhusu haja ya kuweka taifa mbele, kushawishiana kwa hoja kuliko
kulazimisha hoja na haja ya kutunga Katiba itakayoliimarisha taifa letu
na kuendeleza umoja na ustawi wa Watanzania. Sisi wana TANZANIA KWANZA tutaendelea kushawishi kwa hoja na wala hatutalazimisha.
Tatu,
tumeshangazwa na hamaki iliyoonyeshwa na baadhi ya wajumbe wenzetu
kuhusu hotuba ya Rais. Tunasikitishwa na kauli zao zenye mwelekeo wa
kuhujumu mchakato wa kupata Katiba mpya. Viongozi hawahawa
wanaotoa kauli hizi walionekana wakishangilia hotuba ya Rais pale
aliposema yale waliyokuwa wanakubaliana nayo. Iweje watishie vurugu na
kususia kisa tu Rais kasema baadhi ya mambo wasiyokubaliana nayo.
Ustahamilivu wa kidemokrasia, ustaarabu na hekima ya uongozi na utu uzima hautaki hivyo.Hotuba
ya Rais imeweka wazi faida na hasara za mifumo yote ya Muungano wa Nchi
yetu kwa hoja ili Watanzania wawe na fursa pana zaidi ya kutafakari na
mwisho kuamua. Mheshimiwa Rais ametimiza kauli yake ya kushawishi kwa hoja na si kwa kulazimisha.
Nne, Hotuba
ya Mheshimiwa Rais haikuvuruga wala kuingilia mchakato uliopo mbele
yetu. Rais hakuingilia kanuni za Bunge maalum tulizozipitisha, Rais
hakubadilisha Sheria ya mabadiliko ya Katiba, Rais hakupiga kura kwenye
vifungu vya Katiba, Rais ameanza kwa kuipongeza Tume
ya Mh. Jaji Warioba na kuipongeza kw uwasilishaji wake. Alichokifanya
Mheshimiwa Rais kama kiongozi mkuu wa Nchi mwenye hekima na busara na
uchungu wa Nchi yake na kutambua dhamana aliyopewa na Watanzania wote
bila kujali makundi ameelezea faida na hasara za mifumo ya Serikali iliyowasilishwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume. Rais katupa
moyo na kutuhimiza tumalize kazi haraka na tuifanye kwa weledi huku
tukiweka maslahi ya Taifa mbele. Hata pale alipotoa maoni na ushauri
kuhusu baadhi ya vifungu bado Mh.Rais alisisitiza kwamba uamuzi wa mwisho ni wetu sisi Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Tano, dhana ya kuichambua na kuikosoa rasimu maana yake si kumdhalilisha Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe wake. Msingi mzima wa kutolewa Rasimu hii ni kwamba Wananchi tuichambue, tuikosoe, tuirekebishe, tuiboreshe na hata ikibidi tuibadilishe
na mwisho tutaipigia kura sote kwa pamoja. Rasimu haikuletwa kama
Msahafu wala Biblia na ndiyo maana zimewekwa hatua mbili baada ya kazi
ya tume kukamilika: BUNGE MAALUM LA KATIBA na KURA YA MAONI YA WANANCHI.
Rais akiwa mkuu wa Nchi, naye ana nafasi yake katika mchakato wa
Katiba. Sisi wana TANZANIA KWANZA, tunashukuru kwamba Mh. Rais alitutanabahisha
kuhusu maeneo muhimu ya kuzingatia ambayo Tume haikuyaainisha kwa upana
wake ikiwemo mipaka ya Nchi yetu. Tunawapongeza Wajumbe wa tume kwa
kazi waliyoifanya na kuikamilisha. Kazi inayofuatia sasa ni uchambuzi wa
Rasimu waliyoiwasilisha. Katika hatua hii ya sasa ya Bunge la Katiba, Rasimu hii inaweza ikakosolewa na hata
inaweza kubadilishwa sana. Tunawasihi Wajumbe wa Tume waondokane na
dhana kwamba kazi yao inapojadiliwa tofauti na mapendekezo yao siyo
udhalilishaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sita,
Sisi Wajumbe wa Bunge Maalum, wana TANZANIA KWANZA ambao idadi yetu ni
zaidi ya Wajumbe 400 na ambao orodha yetu tutaitoa hivi karibuni kwa
wingi wetu na umoja wetu tunayo dhamira ya
kutimiza wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria na kwa kuzingatia matarajio
ya Watanzania. Tunawasihi wale wenzetu ambao hawakuipenda hotuba ya Mheshimiwa Rais watulie, waondoe hamaki na sote tushirikiane kuifanya kazi hii, kama
wapo ambao kitendo cha Rais kuja kuhutubia na kutoa uchambuzi wake
kuhusu Rasimu, kinawafanya wasitake tena kushiriki katika mchakato huu,
basi uamuzi wao huo waufanye kwa namna ambayo haitatukwaza au kutuzuia
sisi wengine tunaotaka kuendelea na shughuli hii ya mchakato wa Katiba. Tunawasihi
viongozi wa Bunge Maalum wasivumilie wala kuendekeza vitendo vya vurugu
za makusudi vitakavyozuia uendeshaji wa Bunge. Tunawasihi msiruhusu
watu wachache wakaliweka rehani Bunge Maalum ili kutengeneza mtaji wa
kisiasa. Tunawasihi Watanzania wawaone na kuwahukumu wale watakaotaka
kuvuruga au kukwamisha mchakato adhimu wa kupata Katiba mpya kisa tu Mh. Rais kaja kuhutubia Bungeni.
Mwisho, tunapenda kusisitiza kuhusu umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari katika mchakato huu. Hiki ni kipindi muhimu sana katika uhai wa Taifa
letu. Wananchi wengi wanafuatilia mchakato huu kupitia vyombo vya
habari. Tunawasihi wamiliki, wahariri na waandishi wa habari wazingatie
weledi wa hali ya juu sana katika kuripoti mchakato huu. Wananchi
wanapenda kusikia, kuona na kusoma yanayojiri wala sio propaganda za
wanasiasa au makundi mbalimbali. Tunapenda kuvisihi vyombo vya habari
viwaunganishe Watanzania wote katika kipindi hiki muhimu na cha kihistoria. Hata hivyo tunatoa shukrani zetu za dhati kwa vyombo
vya habari na wanahabari wote kwa ushiriki wao katika mchakato huu wa
Katiba. Tunazidi kuwasihi waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa,
kutokufanya kazi kwa kufuata propaganda za kisiasa au kufuata makundi,
kutoa mizania sawa kwa maoni tofauti bila kuegemea maoni ya kundi moja
au matakwa ya makundi fulani kwa kuwa mwisho wa siku sisi sote tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunakuwa na Tanzania moja.
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Libariki Bunge Maalum la Katiba
“TANZANIA KWANZA”
Tunawashukuru kwa kutusikiliza.
Kwa niaba ya Wabunge wa Bunge la Katiba “WANATANZANIA KWANZA”
Said Nkumba, (Mb) Waride Jabu, (Mb)
No comments:
Post a Comment