Pages

Saturday, April 5, 2014

MTAMBO TCRA WABAINI UHALIFU

b2_e5ab2.jpg
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutumia mtambo maalumu uitwao Telecommunication Traffic Monitoring System (TTMS) wamefanikiwa kuwakamata baadhi ya watu wanaofanya udanganyifu katika mitandao ya simu za kimataifa.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema ufungaji wa mtambo huo umeweza kutambua mawasiliano ya udanganyifu katika mitandao ikiwa ni pamoja na namba za ulaghai za nchini zinazotumika kuruhusu au kupitisha mawasiliano ya kimataifa kinyume na matakwa ya sheria. 
Alisema kumekuwa na makampuni na watu binafsi wanaowezesha simu zinazopigwa kutoka nje kufika nchini bila kupitia kwenye njia rasmi, hivyo kuikosesha serikali na makampuni ya simu mapato halisi.
"Watu hawa hutumia internet kuruhusu simu zinazopigwa kutoka nje ya nchi na kuzifanya zionekane kama zimetoka hapa nchini kwa kifaa kinachojulikana kama Sim box," alisema.

Alisema kifaa hicho kina uwezo wa kutumia laini za simu nyingi ambazo zinatumika kuidanganya mitambo ya kampuni za ndani kutokutambua kuwa simu zilizopigwa ni za kimataifa.
" Mwananchi anapopigiwa simu na mtu aliyeko nje ya nchi na akaona kwenye simu yake namba ya mtandao ya hapa nchini ajue kuwa simu hiyo aliyopigiwa inapita kwenye mitandao isiyo rasmi, mara nyingi mitandao hii huwa na huduma mbovu na zisizo na viwango vinavyokubalika," alisema.
Alisema kwa kutumia mitambo hii na kwa kushirikiana na watoa huduma za simu na vyombo vya usalama inafanya uchunguzi wa kitaalamu kila wakati ili kubaini uwepo wa udanganyifu katika mitandao ya simu.
" Zoezi hili ni endelevu na linahusisha ukaguzi na utambuzi wa mitambo inayojihusisha na udanganyifu katika mitandao ya simu na endapo mtu yeyote au kampuni itabainika kuhusika na udanganyifu huu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao," alisema.

No comments:

Post a Comment