Watu wawili akiwemo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya
sekondari Mwigo wilayani Kyela mkoani Mbeya, wanahofiwa kufa maji katika
Mto Kiwira.
Hofu ya kufa maji watu hao inakuja baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia, kupinduka.
Watu
hao walikuwa wakitoka kijiji cha Ibungu kwenda kitongoji cha Ndandalo
kilichopo Kyela. Mto huo unatajwa kujaa maji, kutokana na mvua nyingi
zilizonyesha ukanda wa juu.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi
baada ya kutokea ajali hiyo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Ndandalo,
Lameck Mbembela alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 10.30 jioni.
Mwenyekiti
huyo alisema wakiwa katikati ya mto, mtumbwi uliyumba kutokana na udogo
wake, ikilinganishwa na wingi wa maji yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi.
Watu hao walitumbukia mtoni na katika harakati za kujiokoa, watu
watatu akiwemo mwongozaji walifanikiwa kujiokoa na kushindwa kuwaokoa
wenzao, ambao wanadaiwa hawakujua kuogelea.
Mbembela alitaja watu
wanaosadikiwa kufa maji ni Mzee Akupenda (70), mkazi wa kijiji cha
Ibungu na Stevin Stivin (15), mkazi wa Kyela, aliyekuwa anasoma kidato
cha kwanza katika shule ya Sekondari Mwigo.
Mtoto huyo alikuwa akienda kumsalimia shangazi yake, anayeishi kitongoji cha Kyela Kati kilichopo ng'ambo ya mto huo.
Juhudi
za kutafuta miili ya watu hao zinaendelea. Alitaka wananchi wanaotumia
njia hiyo ya mitumbwi, waache na badala yake watumie njia kuu yenye
daraja kubwa la kijiji cha Ipyana.
Mbembela aliitaka serikali kupitia
halmashauri ya wilaya, kujenga daraja katika mto huo, ambao hutumiwa
na watu wengi kufuata huduma za msingi mjini Kyela.
No comments:
Post a Comment