Dar es Salaam. Ndoto ya Yanga ya kutaka kuongezewa eneo la kujenga uwanja wake Jangwani imegonga mwamba baada ya Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) kudai eneo ni hatarishi.
Habari za uhakika ilizozipata gazeti hili kutoka
kwa moja wa viongozi kutoka NEMC zinasema kuwa katika mapendekezo yao
kwa Kamati ya Mazingira Manispaa ya Ilala wamependekeza Yanga wasipewe
eneo hilo kwa vile ni hatarishi na ni mkondo wa upumuaji wa bahari ikiwa
ni pamoja na mto mkubwa wa Msimbazi.
“Manispaa haina tatizo inasubiri tu tamko la NEMC
kimaandishi pamoja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi, kama Yanga
wapewe kibali au la, lakini NEMC walishasema wazi Yanga wasipewe kibali
kwa vile eneo lile ni hatarishi pia lina matatizo makubwa.
“Kuacha Bonde la Mto Msimbazi, pamoja na mkondo
wa upumuaji wa bahari, kuna mabomba pale lile linalopeleka maji
Hospitali ya Muhimbili na lingine linalopeleka maji baharini,
haiwezekani kwa Yanga kuongezewa eneo kwanza hapo walipo wanatakiwa
waondoke lile ni eneo hatarishi.
“Kuna kituo cha mabasi yaendayo kasi kipo pale
kile sio cha muda ni cha kudumu, sijui ni nani aliyewambia kile ni kituo
cha muda, kuna mlolongo mrefu sana, na Yanga wameshambiwa wakubaliane
na ushauri wa Serikali watafute eneo jingine kwa ajili ya ujenzi wa
uwanja wao, kwa pale haiwezekani,” alisema kigogo huyo.
Akizungumzia suala hilo Mwenyekiti wa Kamati ya
ujenzi wa uwanja huo wa Yanga, Francis Kifukwe alionyesha kushangazwa na
kudai kuwa hana taarifa zozote.
“Huyo mtu anayesema tumenyimwa eneo ni muongo,
barua ya NEMC ambayo walituandikia mwaka jana mbona hawajatuambia hivyo,
kuna masharti ambayo wametupa wakasema tukitekeleza kila kitu kitaenda
sawa.” alisema Kifukwe ambaye hata hivyo hakutaka kuweka wazi masharti
hayo waliyopewa.
Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Manispaa ya
Ilala ilikutana hivi karibuni kujadili suala hilo ambalo hata hivyo
wameliacha suala hilo mikononi mwa NEMC.
Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Manispaa ya
Ilala ilifanya ziara ya ukaguzi Jangwani hivi karibuni kuangalia eneo
linaloombwa na klabu ya Yanga kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wake wa
kisasa.CHANZO MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment