Daktari Luvanda kutoka hospitali ya wilaya ya Makete akionesha majeraha ya kichwa cha mwili wa marehemu yanayohisiwa kupelekea kifo chake.
Polisi kutoka kituo cha Tandala na Makete wilayani wakichukua taarifa za mauaji hayo kwenye shamba ulipokutwa mwili wa marehemu.
Askari akizungumza na wananchi waliofika eneo la tukio na kuwaonya kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi pamoja na kushirikiana na jeshi hilo kuwapata watuhumiwa wa mauaji hayo.
Mkazi wa kijiji cha Masisiwe kata ya Ukwama Wilayani Makete Mkoani Njombe amefariki Dunia baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mguuni na mtu/watu wasiojulikana mwishoni mwa wiki iliyopita
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa niaba ya mkuu wa polisi wilaya, Mrakibu mwandamizi wa Polisi ambaye pia ni afisa upelelezi Wilaya ya Makete Bw.Gozbert Komba amesema walipokea taarifa ya mauaji hayo kutoka kwa uongozi wa kijiji hicho na kumtaja marehemu kuwa ni Masori Sanga(60) mkazi wa kijiji cha Masisiwe Kata ya Ukwama Wilayani Makete
Bw. Komba amesema kuwa marehemu huyo aliuawa usiku wa kuamikia Ijumaa wiki iliyopita na watu wasiojulikana kwa imani za kishirikina kwa kuwa marehemu alikuwa mzee na pia kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda wa tukio hilo waliohojiwa na polisi
Pia amesema mpaka sasa Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi kwa ajili ya kuhakikisha wahusika wote wa tukio hilo wanakamatwa kwani kitendo walichokifanya ni cha kinyama na baada ya tukio hilo muuaji/wauaji hao walitokomea kusiko julikana
Bw.Komba amekemea vikali suala la wananchi kujichukulia sheria mkononi wilayani hapo na kuwaomba wananchi wasiwe na tabia hizo za kuwaua wazee kwa imani za kishirikina na kuwataka watii sheria bila shuruti ili kuishi kwa Amani katika wilaya yao na nchini kwa ujumla
Mwili wa marehemu ulikutwa kwenye shamba la mahindi ukiwa na majeraha sehemu za kichwani na mguuni ambayo yanadhaniwa kusababisha kifo chake, baada ya watu kupita eneo hilo na kuukuta mwili huo
katika kipindi cha hivi karibuni wilayani Makete kumekuwa na matukio ya mauaji kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo wivu wa kimapenzi na imani za kishirikina jambo linalotia doa wilaya hiyo kutokana na ongezeko la watu kuchukua sheria mikononi kwa kuwaua watuhumiwa wa matukio mbalimbali
Habari/picha na Edwin Moshi, Eddy Blog.
No comments:
Post a Comment