Pages

Monday, April 7, 2014

UKATILI WA KUTISHA::MFANYABIASHARA WA BUCHA AMCHARANGA MAPANGA MFANYAKAZI WAKE BUCHANI HUKO MBEYA.

Sunday Mwambelo baada ya kucharangwa mapanga na bosi wake ndani ya buncha eneo la Sae Jijini Mbeya
Ndugu jamaa na marafiki wa Sunday Mwambelo wakimjulia hali katika hospitali ya rufaa Mbeya alikolazwa baada ya kucharangwa mapanga na bosi wake aliyefahamika kwa jina la Simon Njangaje
Sunday Mwambelo akijuliwa hali na dada yake Never Mwambinga katika hospitali ya Rufaa Mbeya alikolazwa baada ya kucharangwa mapanga na bosi wake


WAKAZI wa kitongoji cha Sae Jijini Mbeya hivi karibuni walimuokoa na kifo mfanyabiashara wa bucha katika buncha ya Simon Butchery iliyopo Sae Jijini Mbeya, Sunday Mwambelo ambaye alifungiwa katika bucha na kucharangwa mapanga na watu wawili waliofahamika kwa majina ya Simon Njangale na Daud Edson.

Hatua hiyo ilifuatia tukio la kutisha ambalo lilikuwa linaendelea katika moja ya vyumba vya bucha la nyama ambapo watu watatu walifika eneo hilo majira ya saa 1:00 jioni na kuufunga mlango wa bucha hiyo kwa nje kisha wakaanza kumcharaza mapanga muuza nyama huyo.

Ilidaiwa kuwa mara baada ya watu hao kuingia katika bucha hilo walizima mshumaa ambapo mmoja wao alibaki mlangoni na wawili kati yao waliingia buchani  na kuchukua panga na shoka kisha kuanza kumuadhibu Sunday ambaye ndiye muuzaji wa nyama katika bucha hiyo.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa mmoja kati ya watu hao ndiye mmiliki wa bucha hiyo na kuwa walifikia hatua hiyo baada ya mfanyakazi wa buchani hapo kuingiza hasara ya sh.25,000 ambazo ni sehemu ya fedha za mauzo ya siku hiyo.

Kwa mujibu wa Mwambelo ambaye amedumu katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 10 ni kwamba mara baada ya kuulizwa kuhusu hasara ya kiasi hicho cha fedha alimwambia tajiri yake kuwa atafidia hasara hiyo kesho yake  jambo ambalo tajiri wake hakukubaliana nalo na hivyo kuchukua uamuzi wa kumkata kwa mapanga na kusababisha damu nyingi kumwagika buchani.

''Ghafla walianza kunikata kata kwa mapanga, nikaishiwa nguvu nikakaa chini huku damu zikinivuja, wasamaria wema waliingia kuniokoa,'' alisema Mwambelo kwa taabu kutokana na maumivu aliyonayo.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa baada ya kusikia purukushani katika bucha hiyo waliamua kusogea na kuona dalili za mtu kupigwa ndipo walipoingia na kumuokoa kijana huyo na baadaye kuwapeleka kituo cha polisi huku majeruhi akikimbizwa hospitali.

''Wananchi walifika na kumuokoa Sunday wakaanza kuwapa kipigo wale jamaa, wakawachukua hadi kituo cha Polisi cha Kati na jamaa wakawekwa ndani,''alisema dada wa majeruhi Never Mwambinga.

Never alisema kuwa  jamaa hao walidhamiria kumuua nduguyake kwani hatua ya kumcharanga kwa mapanga huku wakiwa wamezima mshumaa na kufunga mlango ilikuwa inaashiria dhamira mbaya.

Aidha Jeshi la Polisi  kupitia kwa mmoja wa Ofisa wa ambaye kutokana na taratibu za Jeshi hilo sio msemaji wa Polisi alisema kuwa watu wawili ambao ni  Simon Njangale mmiliki wa bucha na mtu mmoja Daud Edson wanashikiliwa kufuatia  tukio hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea   kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani.

Chanzo: MKWINDA BLOG

No comments:

Post a Comment