Pages

Friday, April 4, 2014

Waandishi wawili wauawa Afghanistan

Shambulio Khost, Afghanistan
Waandishi wawili wa habari wanawake wa kigeni wameuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja aliyekuwa amevalia sare za polisi mashariki mwa Afghanistan.
Habari kutoka Afghanistan zinasema mmoja wa wanawake hao alifariki dunia, na mwingine alijeruhiwa vibaya.
Tukio hilo limetokea katika mji wa Khost karibu na mpaka wa Afghanistan na Pakistan.
Tukio hilo limekuja wakati Afghanistan ikiimarisha ulinzi kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais Jumamosi ikiwa ni kukabiliana na vurugu za wapiganaji wa Taliban.
Rais mpya atamrithi rais wa sasa Hamid Karzai, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 ulipoangushwa utawala wa Taliban, lakini kikatiba anazuiwa kugombea kipindi cha tatu cha uongozi.
"Waandishi wa habari wawili wanawake wameuawa kwa kupigwa risasi asubuhi leo ndani ya eneo la makao makuu ya polisi, ambapo wengine wamejeruhiwa vibaya," msemaji wa jimbo la Khost Mobarez Mohammad Zadran ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP.
Amesema kuwa mtu huyo mwenye silaha alikuwa amevalia sare za polisi.
Kundi la Taliban limeongeza mashambulio katika wiki za hivi karibuni, ili kuharibu maandalizi ya uchaguzi.
Mwezi uliopita mwandishi wa habari mwandamizi wa shirika la Agence France-Presse, Sardar Ahmad, aliuawa pamoja na watu wengine nane, wakati wapiganaji wa Taliban waliposhambulia hoteli moja ambayo hukaliwa na raia wengi wa kigeni mjini Kabul, Afghanistan.

No comments:

Post a Comment