Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) akijibu maswali ya waandishi wa magazeti ya Mwananchi Communications Limited nje ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema Rais Jakaya Kikwete hana uwezo kisheria wa kuwafukuza au kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Werema alisema Sheria namba 8 ya Mabadiliko
ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala hilo na kwamba kwa maana hiyo
Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale aliowateua kupitia
kundi la wajumbe 201.
“Umesoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba? Kaisome
maana ili mtu afukuzwe ubunge lazima apungukiwe sifa za nafasi hiyo,
lakini kama sheria iko kimya maana yake ni kwamba hana (Rais) uwezo wa
kuwafukuza,” alisema Jaji Werema.
Jaji Werema alikuwa akijibu maswali ya gazeti hili
kuhusu hatima ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ambao Jumatano jioni waliondoka bungeni kwa madai ya
kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge Maalumu.
Wajumbe waliotoka nje ni wanaotokana na vyama vya
CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, NRA, NLD na baadhi kutoka kundi la 201.
Alhamisi asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alisema
utafiti uliofanywa na ofisi yake ulibaini kuwa katika kundi la 201, ni
wajumbe 25 tu ambao walitoka nje pamoja na Ukawa.
Baada ya wajumbe hao kutoka nje, Mjumbe wa Bunge
hilo, Mwigulu Nchemba ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, aliomba
mwongozo akihoji iwapo Ofisi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu haiwezi
kumwandikia Rais Kikwete ili ateungue uteuzi wa wajumbe katika kundi la
201 ambao waliungana na Ukawa kususia vikao.
“Ningependa Rais atengue hadhi zao ili kuingiza
watu wengine ambao wako tayari kufanya kazi hata bure, sisi tunalipwa
fedha nyingi, lakini tunaleta mzaha, watu hawana maji, dawa, madawati,
ada za elimu ya juu watu wamekosa, hizi fedha zingetumika huko,” alisema
Nchemba mwenye wadhifa mwingine wa Naibu Waziri wa Fedha.
Matakwa ya Sheria
Jaji Werema alisema: “Ili mtu aondolewe katika
nafasi yake ni lazima akose sifa za kuwa mjumbe, mathalan kuugua ugonjwa
wa akili au kichaa, kuumwa muda mrefu kiasi cha kushindwa kutimiza
majukumu yake na kadhalika, lakini sifa hizo kama hazipo kwenye sheria
sasa unaanzia wapi?”
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011 pamoja na
marekebisho yake ya 2012 na 2013 inawataja Wabunge wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa Wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba kwa mujibu wa nafasi zao.
Kadhalika sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya
kufanya uteuzi wa wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali, lakini haitaji
sifa wanazopaswa kuwa nazo wajumbe hao.
Jaji Werema alisema hata kama sheria ingekuwa
inaruhusu kufukuzwa au kusitishwa kwa ujumbe wa wabunge hao, hakuna
sababu ya msingi ya kuwachukulia hatua hiyo.chanzo Mwanainchi
No comments:
Post a Comment