Morogoro. Hali ya mtoto Nasra Rashid
(4) aliyekuwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka minne, imebadilika ghafla juzi
na jana kuwalazimu madaktari kumweka katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu.(Martha Magessa)
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Mkoa wa
Morogoro, Dk Rita Lyamuya alisema jana kuwa tatizo kubwa la mtoto huyo ni
kubadilika ghafla kwa upumuaji wake na utaratibu unafanyika ili leo asafirishwe
kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
"Tunatarajia kumpeleka
Muhimbili mapema asubuhi kwa gari maalumu la wagonjwa ili kupata matibabu
zaidi," alisema Dk Lyamuya.
Alisema juzi Nasra alikuwa mwenye
furaha na mchangamfu lakini jioni yake hali ilibadilika katika mfumo wake wa
kupumua.
Alisema kwa msingi huo, uongozi wa
hospitali ya mkoa umeamua kumsafirisha kwenda katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Uchunguzi wa awali wa afya ya Nasra ulibaini
kuwa mtoto huyo alikuwa na maradhi ya nimonia (kichomi), mifupa ya miguu na
mikono kuvunjika pamoja na utapiamlo.
Watuhumiwa kortini
Katika hatua nyingine, watu watatu
akiwamo baba mzazi wa Nasra, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro
kujibu mashtaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Baba wa mtoto huyo Rashid Mvungi
(47), mama mlezi wa Nasra, Mariamu Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30),
walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo jana na kusomewa mashtaka
hayo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera
alidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Desemba, 2010 na Mei mwaka
huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Alidai kuwa katika kipindi hicho
walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na
hivyo kumsababishia magonjwa.
Alitaja maradhi yaliyomkumba akiwa
ndani ya boksi ni utapiamlo, kichomi na mvunjiko wa mifupa.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment