Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi yenye jumla ya Shilingi 1,219,717,592,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Hatua hiyo ya Bunge kupitisha Bajeti hiyo itawezesha Wizara ya Ujenzi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuendeleza Sekta ya Ujenzi hapa nchini.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti hiyo jana, Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (Mb), alieleza kuwa kati ya fedha hizo Shilingi 557,483,563,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha Shilingi 24,338,319,000.00 za mishahara ya Watumishi (PE), Shilingi 6,944,846,000.00 za matumizi mengineyo (OC) na Shilingi 526,200,400,000.00 kwa ajili ya Mfuko wa Barabara.
Akifafanua kuhusu bajeti ya Maendeleo iliyotengewa Shilingi 662,234,027,000.00, Mhe. Magufuli ameeleza kuwa, kati ya fedha hizo Shilingi 450,000,000,000.00 ni fedha za ndani za miradi ya maendeleo na Shilingi 212,234,027,000.00 ni fedha za nje za miradi ya maendeleo.
Wizara ya Ujenzi ina majukumu yafuatayo, Kusimamia Sera za ujenzi na usalama barabarani, Ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na vivuko.
Pamoja na majukumu hayo Wizara pia inasimamia ukarabati wa majengo ya Serikali, huduma za Ufundi na umeme, kusimamia shughuli za usajili wa Makandarasi, Wahandisi, Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Usalama barabarani na mazingira katika sekta hiyo.
Pia Wizara inasimamia uboreshaji, utendaji na uendelezaji wa watumishi wa Wizara pamoja na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wakala,Taasisi na Bodi zilizo chini ya Wizara.
No comments:
Post a Comment