Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, May 11, 2014

DAKTARI AELEZA ALIVYOUGUA HOMA YA DENGUE


Dar es Salaam. Daktari wa Hospitali ya Mwananyamala, Saleh Kijangwa amejitokeza na kueleza jinsi alivyougua homa ya dengue ambayo imeukumba Mkoa wa Dar es Salaam.


“Niliumwa sana, nikadhani ni malaria na nikahisi imekuwa kali kiasi hicho kwa sababu sikuwahi kuugua malaria maishani mwangu. Nilipima magonjwa mengi lakini hakuna kilichoonekana,” alisema.
Dalili alizoona
Dk Kijangwa alisema alianza kuhisi maumivu makali ya kichwa usiku wa Ijumaa Kuu yaliyoambatana na maumivu ya misuli na viungo vya mwili na joto la mwili kuwa kali isivyo kawaida.
 “Niliumwa sana kichwa, misuli, mgongo, kiuno na shingo. Maumivu yalikuwa makali kiasi nilishindwa kupata usingizi, wakati huo joto lilikuwa kali sana.”
Daktari huyo alisema kosa alilofanya ni kuamua kujitibu kwa kunywa dawa ya maumivu aina ya diclofenac ambayo kwa kawaida haipatani na maradhi hayo.

 
“Diclofenac ina tabia ya kuingiliana na utendaji kazi wa chembe hai hizo, hivyo mtu mwenye dengue akizinywa huathirika zaidi. Kujitibu ni kosa tunalolifanya mara nyingi. Ndiyo maana tunatakiwa tupime kwanza kabla ya kumeza dawa ya aina yoyote,” alisema.
Dk Kijangwa alisema alibainika kuwa na homa hiyo siku tano baada ya kuanza kuona dalili na kwa kuwa dengue haina tiba, alitibiwa kwa paracetamol na kutakiwa kunywa maji kwa wingi.
Kilichosababisha maambukizi
Dk Kijangwa alisema anahisi kilichosababisha yeye pamoja na wakazi wengi wa Wilaya ya Kinondoni kupatwa na ugonjwa huo ni uwepo wa bwawa la maji maeneo ya Kambangwa ambalo huenda ndicho chanzo cha mazalia ya mbu anayeambukiza maradhi hayo, Aedes Egyptiae.
Mpapai wadaiwa kutibu dengue
Baadhi ya ripoti zimeonyesha kuwa majani ya mpapai yana uwezo wa kutibu homa ya dengue. Ingawa haijathibitishwa lakini historia inaonyesha kuwa majani ya mpapai yanatibu ugonjwa huo baada ya kulipuka mara kwa mara nchini India.
Majani ya mpapai hayana madhara na wala si sumu pale yanaponywewa na yamekuwa pia yakitumiwa kwa chakula nchini.
Tafiti zilizowahi kuchapishwa na Jarida la Archieve la India limeeleza kuwa juisi ya majani ya mpapai ilisaidia wagonjwa watano waliopata homa ya dengue kuongeza chembechembe zinazohusika na kuganda kwa damu ndani ya saa 24.
Tafiti nyingine zilizofanywa na madaktari na watafiti kutoka Marekani na Japan na kuchapishwa katika Jarida la Ethnopharmacology zilieleza kuwa juisi ya majani hayo ilionyesha kuwasaidia wagonjwa wa homa ya dengue na ilionyesha kuwa na uwezo wa kutibu malaria na saratani.
Daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Vinitah Saini alisema baadhi ya maeneo wanatumia juisi ya majani ya mpapai kutibu ugonjwa huo lakini akasema hakuna ushahidi wa kisayansi  kuwa yanatibu. (CHANZO: MWANANCHI)(FS)

No comments:

Post a Comment