Pages

Saturday, May 24, 2014

HARUSI YA MBUNGE MAARUFU WA VITI MAALUM CCM VICKIE KAMATA AUGUA GHAFLA NA KULAZWA HARUSI YAKE YA LEO YAAHIRISHWA

Mbunge Vicky Kamata akiwa amelazwa Hospitali ya Tabata General, Dar es Salaam jana



Dodoma/Dar es Salaam. Ni matukio nadra kutokea katika maisha, lakini haya ndiyo yaliyomkuta Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata, baada ya kuugua ghafla saa 36 kabla ya harusi yake.
 
Kuugua kwa bibi harusi huyo mtarajiwa, kumezua gumzo katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na maeneo mengine nchini, kutokana na kile kilichoelezwa kwamba harusi hiyo ilipangwa kuwa ya kifahari ikitarajiwa kutumia Sh96 milioni.
Kamata ilikuwa afunge ndoa leo katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza Dar es Salaam na tayari kadi za mialiko zilishasambazwa kwa watu mbalimbali wakiwamo wabunge.
 
Habari za kuugua ghafla kwa mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa muziki aliyetamba na kibao chake cha ‘Wanawake na Maendeleo’ zilianza kuzagaa kwa kasi juzi jioni nchini.
 Kamata ambaye pia ni mtetezi wa haki za wanawake,  aliugua usiku wa kuamkia jana na kupelekwa katika Hospitali ya Tabata General, iliyopo Segerea ambapo amelazwa.
“Niliugua tumbo ghafla, nilipata maumivu makali sana nikampigia daktari wangu na nilipomweleza jinsi ninavyojisikia, aliniambia niende hospitali haraka na kutokana na hali ilivyo, waliamua nilazwe,” alisema Kamata akiwa kitandani katika hospitali hiyo.
 
Kamata alifafanua kuwa, pamoja na mambo mengine, hali yake ya ujauzito imekuwa ikimsumbua na kuchangia yeye kulazwa kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha wiki mbili. Mbunge huyo ambaye alitakiwa kufunga ndoa leo, alisema kuwa kutokana na maradhi hayo, haelewi hatima ya ndoa yake, ingawa wanafamilia na wanakamati wanaendelea na mipango ya harusi kama ilivyopangwa. “Mama anaenda nyumbani sasa hivi kuniandalia nguo na kila kitu, lakini sijui itakuwaje kwa sababu daktari amesema kutokana na hali yangu ilivyo, itakuwa vigumu kuvaa viatu virefu na kupata usumbufu wote wa purukushani za harusi,” alisema.
 
Aliongeza kuwa mipango yote ya harusi ipo tayari kinachosubiriwa na siku yenyewe, lakini kwa bahati mbaya jambo hilo limetokea na haliwezi kuepukika.
Vicky alisema wanakamati wa Dar es Salaam na wale wa Dodoma, wanaendelea na vikao ingawa, wamechanganyikiwa  kutokana na sintofahamu iliyopo, kama harusi itafanyika au haitafanyika. Ndugu wa mbunge huyo akiwemo mama yake mzazi Kamata walionekana hospitalini hapo  wakiendelea kumfariji na kujadili kuhusu hatima ya harusi hiyo, iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na wanafamilia wote.
 
Daktari wa Kamata, aliyefahamika kwa jina la Diwani Msemo, alieleza kuwa mbunge huyo alifika hospitalini hapo akiwa na maumivu makali ya tumbo yaliyofanana na uchungu wa kuzaa, hali iliyoonyesha kuwa ujauzito wake unatishia kutoka.
“Ukipata yale maumivu kama mimba ni changa inakuwa kama tishio la mimba kutoka, siyo hivyo tu, bali alikuwa anatapika na presha ikashuka. Kwa kweli mimba yake  ipo katika hatari,” alisema Alisema pamoja na kumpa matibabu, walishauriana kuwa apumzike kwa siku tano ili kuhakikisha kiumbe kilichopo tumboni kipo salama.
 
“Ilikuwa ni uamuzi mgumu kwa sababu ni siku yake ya harusi, lakini tunaangalia umuhimu wa kiumbe na kama ataenda, itabidi asaini ili ijulikane kuwa hatukumkubalia. Kwa kifupi hayuko fiti kwa shughuli hiyo,” alisema.
 
Harusi ya Kamata iliandikwa pia na mitandao mbalimbali ya kijamii nchini na jana redio moja ilitangaza kuugua kwake, ikisema kumetokana na matatizo ya ujauzito.
Kumekuwa na uvumi unaosambazwa kwa kasi juu ya sababu za kuahirishwa kwa harusi hiyo, lakini kwa sababu ya maadili ya uandishi hatutaweza kuziandika katika gazeti hili.
Paroko aliyekuwa afungishe ndoa anena
 
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi , Sinza Dar es Salaam, Cuthbert Maganga alipohojiwa kuhusu taarifa za kufungwa kwa ndoa hiyo, alikiri kwamba iliandikishwa ili ifungwe kanisani hapo.
Hata hivyo akasema ilishindikana, baada ya wahusika kukwama kuwasilisha baadhi ya nyaraka muhimu zilizohitajika, ili kukamilisha sakramenti hiyo. 
 
“Ilitarajiwa kufungwa Mei 24 mwaka huu yaani  kesho (leo), lakini kwa taratibu za kanisa letu ilishindikana kwa sababu bibi harusi alishindwa kuwasilisha cheti chake cha ubatizo, pia hakuwa amepata kipaimara, vitu hivyo ni miongoni mwa vitu muhimu vinavyohitajika ili kukamilisha Sakramenti ya Ndoa,” alisema Padri Maganga.
 
Alisema Kamata ndiye aliyekwenda kuandikisha ndoa hiyo, kwa kuwa ni muumini wa kanisa hilo anayetokea Kanda D.
Juhudi za kumtafuta bwana harusi, Charles Gardner hazikuweza kufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakuwa tayari kujibu.
Hata hivyo, baadhi ya rafiki wa karibu wa Gardner walieleza kuwa wamejulishwa kuwa ndoa hiyo haipo na kwamba jana bwana harusi huyo mtarajiwa alionekana akiwa katika hali isiyo ya kawaida.
 
“Nilijaribu kumuuliza kuhusu harusi yake, lakini hakuwa tayari kunieleza bayana, ila hayupo katika hali yake ya kawaida,” alisema mmoja wa rafiki zake.

No comments:

Post a Comment