Tangazo lililobandikwa na Jiji kusitisha zoezi la ukusanyaji wa tozo/vibali vya kuingia mjini na pikipiki.
Baadhi ya madereva wa pikipiki wanaozitumia kama vyombo vya usafiri binafsi kwenda na kurudi kazini wakihoji juu ya mkanganyiko huo katika ofisi za Jiji la Dar es Salaam, juzi. Hata hivyo hawakupata majibu zaidi ya kukuta tangazo lililositisha upokeaji wa toza za kuingia mjini na vibali.ZOEZI la kupiga marufuku bodaboda na bajaji zinazofanya biashara katikati ya Jiji la Dar es Salaam limegeuka biashara kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hasa kwa watumiaji wa pikipiki hizo kwa ajili ya usafiri binafsi wa kawaida kwenda na kurudi kazini, pamoja na makampuni yanayotumia chombo hicho cha usafiri.
Halmashauri ya jiji sasa imeanza kuwatoza watu binafsi na makampuni yanayotumia chombo hicho shilingi 500 kwa siku kila bodaboda inapoingia mjini wakidai ni tozo ya chombo hicho kupata idhini ya kuingia mjini kwa kila siku.
Wakizungumza na mtandao huu jana baadhi ya wananchi wamelalamikia kitendo cha Halmashauri ya Jiji kugeuza zuio la kufanya biashara ya bodaboda katikati ya jiji aina ya biashara ya kujipatia fedha kwa kutoza shilingi mia tano kwa siku kwa kila pikipiki za watu binafsi na makampuni zinapoingia mjini.
Mkazi wa Jiji, Jackson Chalamila alisema tayari amelipia kibali cha miezi sita yaani shilingi 90,000 kama tozo ya kuingia mjini kila siku na ameruhusiwa kuingia mjini na pikipiki yake anayodai huitumia kama chombo cha usafiri kwenda na kurudi kazini kila siku za kazi.
"...Binafsi nimelipia kutokana na usumbufu ambao ninaupata toka kwa mgambo wa jiji kila siku wanatukamata ukiwaonesha kitambulisho cha kazi kinachokuonesha kuwa wewe hufanyi biashara ya bodaboda hawakitambui na wanasema unatakiwa kuwa na kibali, hivyo nikalazimika kukata baada ya kulipia shilingi 90,000," alisema Chalamila.
Aliongeza kuwa hata hivyo utaratibu huo si wa haki bali ni namna ya kuwanyonya wananchi kwani mtu hawezi kulipishwa tozo za kuingia mjini kwa chombo anachokitumia kama usafiri wake wa kwenda na kurudi kazini, ilhali magari hayalipi tozo yoyote ya kuingia mjini.
"Huu ni utapeli mtupu, sisi tunalipa kodi kama ilivyo kwa magari binafsi na ni chombo cha moto mtu unakitumia kama usafiri wako iweje ulipishwe kila siku unapoingia mjini? Mbona watu wanaotumia magari kama usafiri binafsi hawalipi wanapoingia mjini? Huu ni wizi...," alisema.
Mwandishi wa habari hizi alifika hadi ofisi ya Jiji kutaka kupata ufafanuzi juu ya malalamiko hayo ya baadhi ya wafanyakazi wanaotumia pikipiki kwa ajili ya shughuli zao binafsi na kutozwa ushuru wa kuingia mjini, lakini haikufanikiwa kumpata msemaji wa jiji ambapo walizi walidai ametoka nje ya ofisi kikazi.
Mwandishi wa habari hii alishuhudia tangazo lililowekwa na Jiji la kuwarifu wananchi kuwa limesitisha malipo ya tozo za pikipiki kuingia mjini hadi hapo itakapotangazwa tena, ili kutoa nafasi kwa jiji kukagua vibali vilivyotolewa na kuvihakiki kabla ya kuendelea. Hata hivyo baada ya mkanganyiko huo baadhi ya watu waliolipia walianza kufika katika ofisi hizo wakitaka kurejeshewa fedha zao na wengine kuhoji kadhia hiyo. Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment