Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, May 13, 2014

Kashfa Hospitali ya Ocean Road,Mgonjwa apewa Dawa Feki Tena kwa Malipo kwenye Akaunti y Mtu Binafsi


Dar es Salaam. Kashfa imeikumba Hospitali ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kutokana na tuhuma za mmoja wa wauguzi wake kumuuzia dawa 'feki' mgonjwa ambaye anaendelea kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo ya Serikali.
Mtumishi wa ORCI katika kitengo cha dawa, Almasi Matola anatuhumiwa kudai fedha kwa mmoja wa wagonjwa wa satarani (jina tunalihifadhi kwa sasa), lakini akampa dawa feki baada ya kupewa fedha.
Mgonjwa huyo alipewa rufaa kwenda Ocean Road Novemba mwaka jana akitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kubainika kwamba alikuwa na saratani ya titi.
Baada ya kufika ORCI, ilibainika kwamba mgonjwa huyo alikuwa akihitaji tiba ya kuua vijidudu vya saratani inayojulikana kitaalamu kwa jina la chemotherapy au chemo kwa kifupi na ndipo alipokutana na Matola.
"Huyu Almasi (Matola) alisema anahitaji apewe fedha za dawa moja kwa moja kupitia akaunti yake ya NMB yenye namba zinazoanzia 206016024** (namba mbili za mwisho tumehifadhi), ambako tuliweka kiasi cha Sh340,000," alisema mgonjwa huyo.
Almasi alikiri kuwekewa fedha katika akaunti yake, lakini akakanusha kuomba fedha hizo kama ujira wa kumpa mgonjwa huyo dawa.
"Huyo mgonjwa unayemsema ninamkumbuka ijapokuwa jina lake limenitoka. Lakini ni kweli sijawahi kuonana naye uso kwa uso isipokuwa nilikuwa nawasiliana naye kupitia kwa mfanyakazi mwenzangu ambaye ni ndugu yake. Huyo ndiye alikuja kwangu na kutaka nimsaidie ndugu yake," alisema Matola.
Kwa mujibu wa taratibu za OCRI, wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kwa rufaa kutoka hospitali nyingine hawapaswi kutozwa fedha zozote kwa ajili ya matibabu.
Mmoja wa madaktari wa OCRI, Dk Steven Shadrack alisema utaratibu wa wagonjwa wengi waliogundulika na saratani, kwa kawaida hutokea Muhimbili ambako huwa wamefanyiwa uchunguzi.
Dk Shadrack alisema mgonjwa anapopewa rufaa kwenda OCRI, hatakiwi kulipia hata senti tano na kama kuna kifaa kilichoharibika ndipo hutakiwa kupimwa nje ya hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa madaktari, mgonjwa wa saratani anayehitaji tiba ya chemo, hutakiwa kupewa dozi hiyo kulingana na hatua ya saratani na aina ya dawa aliyoandikiwa.
Ilikuwaje
Mgonjwa huyo alisema Matola alimwambia kuwa tiba yake inahitaji dozi sita za dawa ambazo gharama yake ni zaidi ya Sh2 milioni kwa maana kwamba kila dozi inagharimu Sh340,000.
Alisema kabla ya kuanza kupewa tiba, alielekezwa atoe damu kwanza, ambayo ingepimwa na majibu kutoka siku inayofuata, hivyo angeanza kupewa tiba siku ya tatu.
"Siku ya kwanza ilikuwa Novemba 3, 2013 nilipotolewa damu na nikaenda siku ya tatu kupewa tiba ya chemo," alisema mgonjwa huyo. Alisema alipokwenda kwa ajili ya kupewa dozi ya pili, Matola alimchukua damu na hapohapo akamwekea dripu ya dawa.
Alisema licha ya kupewa tiba hiyo, alikuwa akisikia maumivu makali kwenye titi lililoathirika huku sehemu ya uvimbe ikitoka damu na maji kwa wingi na uvimbe huo ambao ulikuwa mdogo, uliendelea kusambaa kuelekea mabegani, chini ya kwapa hadi kwenye tumbo. "Nilikuwa kwenye maumivu makali sana. Halafu, ndani ya dakika 10, nguo yangu ilikuwa inalowa kwa maji kutoka kwenye titi," alisema mgonjwa huyo.
Katika awamu ya pili na ya tatu ya tiba, mgonjwa alisema alikuwa akimpatia Matola mkononi Sh340,000 kwa kila awamu na kwamba alikuwa akiweka fedha hizo mfukoni, taarifa ambazo hata hivyo, Matola alizikanusha.
Wasiwasi wa tiba
Kwa maelezo ya Dk Shadrack, kwa kawaida dawa za saratani hasa chemotherapy zina madhara mbalimbali kwa watumiaji wake.
"Kwa mfano, mgonjwa baada ya kupata chemo, anaweza kuharisha, kutapika, damu kupungua na wakati mwingine kupata kizunguzungu," alisema Dk Steven na kwamba dalili kubwa kwa wanaopata tiba hiyo huwa ni nywele kunyonyoka.
Lakini, licha ya mgonjwa huyo kupewa dozi tatu za chemo, hakuwahi kupata athari zozote kama hizo.
Mgonjwa huyo alisema ulipofi ka awamu ya nne ya kupewa dawa hiyo Januari 15 mwaka huu, alimwambia Matola kwamba hali yake inazidi kuwa mbaya hivyo alitaka kwenda kwa daktari bingwa, lakini alimkataza akisema hiyo ni hali ya kawaida tu.
"Baada ya kuniambia hivyo alisema kwa dozi ya nne na kuendelea atanipunguzia bei ya dawa na sasa nitakuwa nikilipa Sh320,000 kwa dozi na kama kawaida nilimkabidhi na akaziweka mfukoni kwake."
Alisema alikwenda kwa daktari bingwa, Dk Dominista Kombe na kumwelezea hali yake. "Ni kama alishtuka hivi na alisema inashangaza kama nilikuwa nimepata dozi nne lakini nywele zangu zilikuwa hazijanyonyoka," alisema
Alisema daktari huyo alionekana kushangazwa na kiasi kikubwa cha fedha alizokuwa akitozwa na kumwagiza amwite Matola.
"Wakati tukielekea kwa daktari, Matola alikuwa akilalamika kwamba 'nimeshaharibu mambo'. Hata hivyo, sikuruhusiwa kuwepo wakati wa mazungumzo kati ya daktari na Matola," alisema.
Alisema baadaye Dk Kombe alimwambia ni vyema aanze tiba upya kwani dawa alizopewa ni feki.
Daktari huyo alimwandikia dawa nyingine na kumwelekeza aende katika duka la dawa ambako alizinunua kwa Sh26,000.
Alisema baada ya dozi ya kwanza tu, aliona dalili zote za kufanya kazi kwa tiba hiyo ukiwamo uvimbe kuanza kunywea, damu na maji kukauka.
Utetezi wa Matola
Lakini Matola alidai kuwa mgonjwa huyo alitoa fedha kama asante.
"Baada ya kuwa nimewapatia dawa, yule mfanyakazi mwenzangu aliniambia kwamba mgonjwa anataka namba yangu ya simu au akaunti ya benki ili anipe asante na mimi niliwapa ila sikujua waliweka shilingi ngapi," alisema Matola.
"Nilipokwenda benki nilikuta fedha zimeongezeka, lakini sikujua ni shilingi ngapi ila yule mgonjwa aliwahi kunipigia simu akaniambia kwamba aliniwekea asante, sijui Sh300,000 au 330,000 au sijui 340,000..."
Matola alisema hakuwahi kumwomba fedha mgonjwa huyo na kwamba hakuwahi kuchukua fedha mkononi kama anavyodai.
Dk Kombe anena
Dk Kombe alikiri kukutana na tukio hilo na kusema baada ya kuona hali ilivyo kwa mgonjwa, alimwandikia dawa nyingine ili aendelee na matibabu.
"Nakumbuka hiyo kesi lakini simkumbuki mtu mwenyewe, ila ninachojua ni kuwa, yeye mwenyewe (mgonjwa) alimpa mtu hela mkononi. Yalikuwa ni makosa yake kwa upande mwingine, dawa hazinunuliwi sasa utampaje mtu hela mkononi?" alihoji daktari huyo.
Dk Kombe, ambaye alisema hakumbuki ni mhudumu gani aliyefanya hivyo, alionyesha kuhofia maisha ya mgonjwa au wagonjwa ikiwa taarifa hizo zitatolewa gazetini.
"Unajua wataendelea kupata tiba kwa muda mrefu hapa na hii ni hatari kubwa kwao, huwezi kujua nini kinaweza kuwapata. Cha muhimu wameandikiwa dawa nyingine na wanaendelea nazo, ni bora wangekaa kimya," Dk Kombe.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Ocean Road, Dk Twalib Ngoma alisema mgonjwa aliyefanyiwa hayo aende kushtaki kwenye vyombo vya sheria badala ya vyombo vya habari.
"Anakuja kwako kulalamika wewe umsaidie nini? Anatakiwa kwenda katika vyombo vya sheria ili apewe haki yake, wewe utamsaidiaje?" alihoji Dk Ngoma.
Alisema kama mgonjwa amefanyiwa unyama kama huo, anatakiwa alipwe fidia na hakuhitaji maswali zaidi ya hapo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Mussa Wambura alisema watashughulikia suala hilo kwa kupata vithibitisho vyote(E.L)Chanzo MjengwaBlog

No comments:

Post a Comment