Pages

Saturday, May 24, 2014

MKWARA WA RAIS WA TFF KUZIFUNGIA TIMU ZA YANGA NA SIMBA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Mohammed Mdose na Said Ally
TIMU za Ligi Kuu Bara zikiwemo Simba na Yanga, huenda zikazuiwa kushiriki kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokana na kutotekeleza agizo la kuwa na madaktari wenye vigezo kwenye timu zao.
Agizo hilo lilitolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa nia ya kuhakikisha kila klabu inakuwa na madaktari waliokidhi vigezo kisha kuwafanyia vipimo wachezaji wao wote kabla ya kuanza kwa ligi.
Imejulikana kuwa, katika agizo hilo, ni klabu moja pekee kati ya 13 ambayo ndiyo imewasilisha kile ilichoagizwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF, Paul Mareale, amesema wamebaini tatizo hilo baada kupitia wasifu wa kila daktari, hivyo kama hawatatimiza kigezo hicho hawatairuhusu kushiriki ligi.
“Kumekuwa na madhara makubwa wanayopata wachezaji kutokana na kutokuwa na wataalam sahihi wa tiba, hatutaki haya yaendelee kujitokeza.

“Msimu huu tupo makini kuhakikisha kila mchezaji hasajiliwi mpaka afanyiwe vipimo vya afya, tena na daktari mwenye viwango vinavyotakiwa na TFF, kwa klabu isiyofuata masharti hayo hatutairuhusu kushiriki ligi kuu.

“Hali hii ya wachezaji kuumia kila siku inatisha, ajabu ni kuwa hakuna klabu iliyoonyesha kujali zaidi ya Azam. Simba na Yanga walitakiwa kuwa mifano lakini wao nao hawajaleta chochote, tutawafungia kwa kuwazuia kushiriki kama wasipotimiza masharti,” alisema.
CREDIT:GPL

No comments:

Post a Comment