Pages

Wednesday, May 21, 2014

MTOTO WA MIAKA 7 AGONGWA VIBAYA NA GARI NA KUFARIKI DUNIA PAPO HAPO WILAYANI KAHAMA

Mwili wa Mtoto huyo ukiwa umefunikwa na kupakiwa ndani ya gari la Polisi

Na Marco Mipawa, Kahama
Mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na Umri wa miaka 7-10 jina na makazi yake hayajafahamika, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akivuka barabara Kuu iendayo Rwanda katika eneo la Nyihogo wilayani Kahama Mkoani Shinyanga. 
Tukio hilo limetokea jana majira ya Saa Nane na nusu mchana likihusisha gari aina ya fuso Mitsubish lenye no T559 Mali ya Kuzenza John,lililokuwa linaendeshwa na dereva Samwel Martine (38). 
Kwa mujibu wa mashuhuda, chanzo cha ajali hiyo ni mrundikano wa magari yanayoegeshwa katika eneo la kisima cha mafuta cha Nyihogo sehemu iliyowahi kusababisha zaidi ya ajali 5 hadi sasa. 

Kufuatia ajali hiyo wananchi walifunga barabara wakishinikiza serikali kuweka matuta pamoja na kuondoa maegesho ya magari yaliyopo katika eneo hilo, ili kuwapa nafasi waenda kwa miguu kuvuka barabara kwa usalama. 

Baadhi ya vipande vya magogo vilivyotumika na wananchi hao kufunga barabara hiyo kuu ya kwenda nchini Rwanda na Burundi
Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani wilayani Kahama Robart Sewando, amesema kwa sasa jeshi la polisi litaimarisha ulinzi katika eneo hilo, ikiwemo kuzuia uegeshaji wa magari wakati taratibu zingine za Serikali zikiendelea. 

Jeshi la polisi wilayani Kahama linamshikilia dereva wa gari hilo Samwel Martine kwa mahojiano,ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Kahama.
Gari ya polisi ikiingia katika hospitali ya wilaya ya Kahama kupeleka mwili huo
Baadhi ya wananchi wakishanga ajali hiyo awali mara baada ya kutokea

No comments:

Post a Comment