Pages

Wednesday, May 7, 2014

MWANAMKE KUWA MAKINI NA MWANAUME MWENYE TABIA HIZI HAWAFAI.



1. Mwanaume Kicheche:
Hakuna mwanamke anayependa kuchezewa na wanaume, labda tu kama anafanya hivyo katika juhudi zake za kujikwamua kiuchumi, lakini pale mwanamke anapokuwa katika harakati za kutafuta mwanaume ambaye kama mambo yakiwa mazuri wafunge ndoa, ni vyema akajiepusha na wanaume vicheche wanaotongoza wanawake kwa lengo la kustarehe na kumaliza matamanio yao ya ngono. wakati mwingine mwanaume mwenye tabia ya kuchezea wanawake anaweza kumfuata mwanamke ambaye ametamani mwili wake na kujifanya eti amebadilika na kuwa mtakatifu. Anaweza kujiweka katika mazingira yanayoonyesha kwamba amebadilika ili kumvuta mwanamke. Shituka mwanamke, jasiri haachi asili atakutumia kama condom na kisha kukutupilia mbali. Wanaume wenye tabia hizo ni vigumu kubadilika. Inahitaji subira ya hali ya juu kujiridhisha kama kweli amebadilika au anazuga ili apate anachokitaka.



2. Mwanaume asiye na kazi na asiyejishughulisha:

Mwaume asiye na kazi na asiyejishughulisha ni mzigo usio na mwenyewe. Mwanaume asiyejishughulisha eti kwa sababu hajapata kazi huyo hana malengo. Kukubali kuwa na uhusiano na mwnaaume wa aina hiyo ni sawa na kuishi na mtu mfu anayetembea (dead alive), labda tu kama atakupa sababu inayoingia akilini kuhusu kutokuwa kwake na kazi na kutojishughulisha kwake. Kama atakuwa ni mtu wa kulalamika tu kwamba hakuna ajira na haonyeshi dalili zozote za kuhangaika kutafuta hata vibarua ili kujikimu eti kwa sababu ni msomi na badala yake anageuka kuwa ombaomba kwa ndugu zake na marafiki zake Nawashauri wanawake muwaepuke wanaume wa aina hii kwani hawafai wanataka kulelewa. Kama amekuona unafanya kazi au una vibishara vyako vinavyokuingizia shilingi mbili tatu zinazokufanya uishi vizuri hapa mjini jua kwamba hicho ndicho kilichomvuta kwako, ukikubali umekwisha maana atakukamua hadi tone la mwisho kisha ahamie kwa mwingine, si kilichomleta kwako hakipo, sasa awe na wewe kwa lipi....



3. Mwanaume asiyejiamini:
Kukubali kuwa na mahusiano na mwanaume asiyejiamini ni sawa na kuishi na bomu ndani ya nyumba. Mwanaume asiyejihisi kuwa yuko salama na mwenye mashaka muda mwingi kuhusu uhusiano wenu, hutawaliwa na wivu wa ajabu ambao licha ya kukuletea fedheha kwa ndugu, jamaa na marafiki zako, lakini pia anaweza kukudhuru au hata kukutoa roho siku moja. Wanaume wasiojiamini mara nyingi ni watu wa kujitilia mashaka kuhusu hali zao za kipato na uwezo wao katika tendo. Kuwa na mahusiano na mwanaume asiejiamini inabidi uishi kwa akili na uchague maneno ya kuzungumza kila uwapo naye, kwani kila neno utakalotamka litatafutiwa tafsiri na kitakachofuata ni tafrani, sasa tabu yote ya nini..... Tupa kule hafai kwa mchuzi wala kwa kulumangia...



4.Mtoto wa mama:

Inawezekana mwanaume akalazimika kuishi nyumbani kwao kwa muda baada ya kumaliza masomo au amepoteza ajira na akawa bado hajapata ajira au hajapata shughuli ya maana itakayomwezesha kujitegemea, hii inakubalika. Hata hivyo kama mwanamke anakutana na mwanaume ambaye anaishi na wazazi wake na haonyeshi dalili za kutafuta kazi au shughuli yenye kipato itakayomwezesha kuondoka hapo kwao na kujitegemea, usije ukajiingiza katika uhusiano na mwanaume wa aina hiyo, itakula kwako, huyo ashakuwa kupe na tegemezi, utakuwa ni mzigo wako na atakuganda kama luba na kupoteza bahati ya kukutana na wanaume wenye mwelekeo wa maisha.



5. Mwanaume anayependa kutukuzwa kama mfalme:

Unaweza kukutana na mwanaume aliyejipachika kibandiko ufalme ambaye anapenda sana kuhudumiwa kama mfalme. Yaani anataka afanyiwe kila kitu, na hajishughulishi kukusaidia kazi hata zile zinazotakiwa zifanywe na mwanaume, yeye kazi yake ni kukaa sebuleni na kuangalia TV au kusoma vitabu au magazeti huku akiagiza kila kitu asogezewe miguuni. Hawezi hata kunyanyuka kufuata kitu anachotaka na badala yake ni kuamrisha aletewe. Mwanaume wa aina hii ni wa kuepukwa kwani mwanamke kukubali kuwa na uhusiano na mwanaume mwenye tabia za kupenda kutukuzwa kama mfalme ni kutaka kuishi kwa msongo wa mawazo na jakamoyo na hivyo kufupisha umri wako wa kuishi hapa duniani. Kinga ni bora kuliko tiba, ukikutana na mwanaume wa aina hii chapa lapa hakufai..



6. Mwanaume mwenye utititri wa watoto kila kona:
Mwanaume kuwa na watoto nje ya ndoa si jambo la kushangaza siku hizi, lakini pale unapokutana na mvulana mwenye umri wa miaka 25 lakini ana watoto watatu kwa mama tofauti, mh! hapo sikushauri ujiingize kwenye uhusiano na mwanaume huyo. Hata hivyo si lazima awe na miaka 25 tu hata mwanaume mwenye umri mkubwa zaidi ya huo halafu ana watoto watatu au hata wanne au zaidi kutoka kwa mama tofauti ni wa kuepuka. Hivi atakupa sababu gani zilizomfanya akawa na watoto kwa mama tofauti kila kona ya mtaa mpaka umuelewe! Kuwa na mahusiano na mwanaume aina hiyo ni kukaribisha shari nyumbani kwako maana kila siku utapata wageni wanaokuja kudai hela za matumizi kutoka kwa mumeo tena wengine watakuja kishari hasa na kukuharibia siku. Mh mh! sikushauri mwanamke, sepa zako, bado nafasi unayo ya kumpata mwanaume mwingine mwadilifu.






7. Mwanaume anayejipenda mwenyewe:

Mwanaume anayejipenda mwenyewe ni kizungumkuti kingine ambacho wanawake wanapaswa kujiepusha nacho. Utakuta mwanaume anajipenda mwenyewe hakuna anachojali kuhusu mwenzi wake zaidi ya kujijali yeye mwenyewe. Wanaume wenye tabia hii ya kujipenda wenyewe, huwa wana kawaida ya kujijali wao wenyewe. Wanataka wavae nguo nzuri za thamani ili wao wapendeze na si wenzi wao. Swala la kumjali mwenzi wake halipo katika vichwa vya wanaume wa aina hii kabisa. Mwanamke sikushauri uingie katika moto huu.



8.Mwanaume bahili:
Unakutana na mwanaume mtoko wa kwanza tu anakuchagulia aina ya chakula au kinywaji kwa kuangalia bei rahisi na wakati wa kulipa anahesabia hela yake mfukoni, huyo ni janga. Utakapoingia katika uhusiano na mwanaume wa aina hii atakusumbua sana na pia katika kupanga bajeti nyumbani usishangae akihesabu finyango za nyama au vipande vya samaki jikoni. Sikushauri mwanamke, we ingia mitini hakufai huyo........



9.Mwanaume chapombe mlevi kupindukia:
Hakuna ubaya mtu kunywa pombe, hasa kama unajua kiwango chako cha unywaji, lakini kuwa na uhusiano na mwanaume mlevi anayekunywa pombe kupindukia kila siku non stop 24/7 huyo hafai. Mwanaume wa aina hii ndio wale wanaosema kunywa pombe watoto wakitembea uchi atajua mama yao. Hata siku moja hawezi kuzungumzia maendeleo kwa ustawi wa familia, kwake utakuwa ni msamiati mgumu.



10. Mwanaume mwenye kisirani na asiyeweza kumuuwa nyoka akafa :

Mwanaume mwenye kisirani ni ngumu sana kuishi naye. Mwanaume mwenye kisirani na anayependa kuweka vitu rohoni na asiyeweza kusamehe ni janga. kuishi na mwanaume wa aina hii ni sawa na kuishi na explosive material ambayo yakipata joto tu hulipuka. Mwanaume umetoka naye mtoko wa kwanza na kwa bahati mbaya mhudumu wa mghahawa akasau kitu katika vitu mlivyoagiza akagomba kupita kiasi na kuwakusanya mameneja wote wa mghahawa akiwemo mpishi mkuu akilalamika. Na kama hiyo haitoshi mtaondoka hapo mghahawani njia nzima kambeba kichwani mhudumu yule masikini aliyeghafilika mpaka mwisho wa safari yenu na huenda akalala naye kichwani. Mwanaume huyo hafai kama gome la mgomba lisilofaa kwa dawa ya miti shamba wala kuni, labda kwa kufungia ugoro. Huyo mpishe ajiendee zake hakufai......

No comments:

Post a Comment