Pages

Saturday, May 24, 2014

RAIA WAWILI WA ROMANIA WAFIKISHWA MAHAKAMANI WAKIKABILIWA NA MASHITAKA 7 YA KUHUJUMU UCHUMI WA TANZANIA


MABOSI wawili wa Kampuni ya X Plora Ltd, raia wa Romania, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka ya kufanya mawasiliano ya simu za kimataifa bila leseni na kuisababishia serikali hasara ya sh.bilioni mbili.Meneja Mtendaji wa kampuni hiyo, Razvan Pantilie (47) na Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Robert Kraus (27), wanaoishi Hoteli ya Serena, walipandishwa kizimbani jana mahakamani hapo.Washitakiwa hao, ambao wanatetewa na Wakili Alex Mgongolwa, walisomewa mashitaka saba na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Isaya Arufani.Kweka alidai washitakiwa walitenda makosa hayo, kati ya Aprili na Mei, mwaka huu, katika ofisi za Raha Data Center, zilizoko maeneo ya Banda la Ngozi, Dar es Salaam.
  1. Kweka alidai katika tarehe tofauti, washitakiwa hao walifanya mawasiliano ya simu za kimataifa kinyume cha sheria kwa kutokuwa na leseni ya TCRA, kwa lengo la kukwepa kodi.
  2. Pia, alidai katika kipindi hicho, washitakiwa hao waliingiza nchini vifaa vya mawasiliano bila kuwa na leseni ya TCRA.
  3. Washitakiwa hao wanadaiwa kuingiza nchini Voice Over the Internet Protocol (VoIP) nne na kuvifunga bila kuwa na kibali cha kuwaruhusu kufanya hivyo.
  4. Pia, washitakiwa hao wanadaiwa kutumia vifaa hivyo vya mawasiliano, ambavyo havijathibitishwa na TCRA.
  5. Katika shitaka la sita, ambalo linamkabili ofisa mtendaji mkuu huyo, anadaiwa alibadilisha usajili wa umiliki wa kadi za simu bila ya kutoa taarifa kwa kampuni husika.
  6. Mshitakiwa huyo anadaiwa alibabadili umiliki wa kadi za simu namba 0776990681 na 07769990758 zilizotolewa na Zantel(T) Ltd na kushindwa kutoa kutoa taarifa ya mabadiliko ya umiliki kwa Zantel alipoihamishia kwa Global Com.
  7. Shitaka la saba la kuisababishia hasara mamlaka husika linawakabili washitakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika kipindi hicho wakiwa hawana leseni, walitumia njia ya mawasiliano bila kibali na kuisababishia serikali na TCRA hasara ya sh. 2,109,888,000.
Hakimu alisema washitakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi hivyo hawatakiwi kujibu lolote.

Wakili wa Serikali alidai upelelezi haujakamilika hivyo aliomba kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Washitakiwa walirudishwa rumande.

Machi, mwaka huu, TCRA ilimpandishwa kizimbani mahakamani hapo, raia wa Kenya, Nelson Rading Onyango, kwa tuhuma za kutoa huduma za simu za kimataifa bila ya leseni na hivyo kuisababishia serikali na TCRA hasara ya sh. bilioni 6.8 .

No comments:

Post a Comment