Pages

Tuesday, May 20, 2014

TAZAMA PICHA NJIWA MWENYE HIRIZI ATIKISA MUHIMBILI WAGONJWA WAHAHA

Njiwa aliyetua kwenye kitanda cha mgonjwa na baada ya muda mgonjwa akafariki.

Hofu kubwa ilitanda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jumatatu ya wiki iliyopita, baada ya Njiwa mweusi, mwenye miguu myekundu akiwa na hirizi iliyofungwa katika mojawapo ya mabawa yake, kutua katika miguu ya mgonjwa aliyekuwa amelazwa wodi namba tatu, jengo la Mwaisela.Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wauguzi wa wodi hiyo ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema tukio hilo lilitokea saa 3.55 asubuhi ambapo njiwa huyo aliingia kupitia dirishani na kwenda kutua mguuni mwa Mwanahawa Ngunda (61) aliyekuwa amelala kitanda namba 7, ambaye anadaiwa kuwa mkazi wa Kimara.
Njiwa huyo aliingia dirishani muda mfupi baada ya mgonjwa aliyekuwa jirani na Mwanahawa, aitwaye Fatuma Musa (45) kurejea wodini hapo akitokea kupata vipimo ambapo alisaidiwa na ndugu zake kupanda kitandani kutokana na kuishiwa nguvu.
Inadaiwa kuwa baada ya kuingia wodini, njiwa huyo alianza kuzunguka na kuleta taharuki kubwa kwa wagonjwa, wauguzi na ndugu waliokuwemo, kiasi cha baadhi yao kukimbia huku wakipiga mayowe, kabla ndege huyo hajaenda kutua miguuni mwa mgonjwa huyo, huku akiwa ametuna na macho yake mekundu yakiwa yanalenga lenga machozi.
Inasemekena baada ya muda, ndege huyo aliruka na kutua dirisha lililokuwa usawa wa kitanda alicholala Fatuma na kuzidi kuwakoroga watu ambao waliamini kuwa ni mambo ya kishirikina. Ndugu wa mgonjwa aliyetuliwa na njiwa huyo, anayedaiwa kuwa ni mama yake mzazi, alikosa amani akiamini jambo baya lingemtokea.
Lakini katika hali ya kushangaza zaidi, mhudumu mmoja wa wodi hiyo alisema wakati watu wakitaka njiwa huyo aondolewe ili kuondoa usumbufu, dada wa Fatuma, aliyejulikana kwa jina la Mwanaisha Musa alimwambia mhudumu kuwa yeye amempenda ndege huyo na anaomba apewe kwani anahitaji kwenda kumfuga.
Kitanda kikiwa tupu baada ya mgonjwa kufariki.
Mhudumu huyo alimweleza dada huyo kuwa anaweza kumchukua kama anaweza, ndipo dada huyo alipomwambia kaka yake aliyetajwa kwa jina la Yasini amkamatie, ambaye alimfuata dirishani na kumkamata bila ndege huyo kuleta ubishi na kumkabidhi dada yake.
Baada ya dada huyo kukabidhiwa ndege huyo na yeye kumfunika na kanga yake kama kichanga, ndipo ndugu wa mgonjwa aliyetuliwa na njiwa huyo alipodaiwa kupandisha mashetani, akimfuata Mwanaisha ambaye alishaanza kutoka wodini hapo.
Ndugu huyo alimfuata akidai kulikuwa na jambo kwani haiwezekani watu wote wamuogope njiwa huyo, lakini yeye amchukue bila hofu.
Inadaiwa kwamba pamoja na mtoto wa marehemu kupiga mayowe lakini Mwanaisha hakuweza kumwachia njiwa huyo. Hata hivyo, mkusanyiko mkubwa wa watu na mayowe, yaliwafanya walinzi kuingilia kati kumtaka mama aliyemchukua njiwa huyo, kumkabidhi kwao mara moja.
Baada ya kukabidhi, Mwanaisha na kaka yake waliondoka na kumuacha ndugu wa mgonjwa akilalamika juu ya usalama wa mama yake, hivyo kuanza kuwapigia simu ndugu na jamaa zake akiwaeleza juu ya tukio hilo.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika wodi hiyo na kukuta kitanda alicholazwa mgonjwa aliyekanyagwa na njiwa akiwa hayupo na alipouliza, wauguzi walisema mgonjwa huyo alifariki siku iliyofuata (Jumanne wiki iliyopita) muda kama uleule wa saa 3.55 ambao njiwa huyo alifika.
Bi. Fatuma akiwa wodini.
Fatuma ambaye bado amelazwa wodini hapo alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kutokea.
“Ni kweli njiwa mwenye hirizi alitokea hapa wodini na alipoingia akamkanyaga mgomjwa mwenzangu, hata hivyo dada yangu alimpenda,
alimuomba mhudumu amruhusu amchukue, alikubaliwa na alipomchukua ndipo mtoto wa marehemu alipandisha mashetani na dada aliamua kuwakabidhi askari,” alisema mgonjwa huyo aliyedai hali yake bado siyo nzuri na kwamba anasubiri vipimo.

 
Habari zaidi zinasema njiwa huyo alitoweka kiaina kutoka mikononi mwa askari wa Muhimbili wakati akishikiliwa katika ofisi kuu ya usalama wakisubiri agizo kutoka kwa viongozi wa juu.

Msemaji mkuu wa hospitali hiyo, Aminiel Akaesha alipohojiwa alikiri kutokea kwa tukio hilo huku baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo wakizungumzia kuhusu uwepo wa ishara ya mambo ya kishirikina wakati mwingine watu wasioonekana wakizungumza hasa katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti.

No comments:

Post a Comment