WAAJIRIWA wapya wa fani ya ualimu wa shule za msingi katika Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga wameanza kazi kwa kuonja machungu ya madeni baada ya kutopewa stahili zao zote kabla ya kuanza kazi na kusambazwa kwenye vituo vyao vya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Wakizungumza na Thehabari.com kwa masharti ya kutotaja majina yao kwa kuhofia kunyanyaswa na uongozi wa juu wilayani hapo, walisema kuwa kwa mujibu wa makubaliano na taratibu walitakiwa kulipwa shilingi 245,000 ikiwa ni malipo ya fedha za kujikimu kwa siku saba yaani shilingi 35,000 kwa kila siku jambo ambalo halikufanywa.
Mmoja wa walimu hao walioanza kazi tangu Aprili Mosi, 2014 alisema walipoanza kazi walilipwa shilingi 140,000 tu na kuahidiwa kiasi kingine kumaliziwa ndani ya mwezi huo, ahadi ambayo haijatekelezwa ilhali wao wakiangaika na maisha ya ugenini fedha hawana na wamepigwa marufuku kufuatilia fedha halmashauri hadi hapo itakapotangazwa.
Alisema walitegemea kwa kuwa malipo ya kujikimu hawakupewa yote wangelipewa mshahara wa mwezi Aprili jambo ambalo nalo halikutekelezwa kwani wamejibiwa kuwa, eti hakuna fedha kwa sasa hadi hapo watakapojulishwa kwenye vituo vyao vya kazi.
"...Wakati tunaanza kazi (Aprili Mosi) tulipewa shilingi 140,000 badala ya Shilingi 245,000/- tuliahidiwa tungelipwa malipo yaliobaki ndani ya mwezi wa nne lakini hadi leo hatujalipwa na tumezuiwa kwenda kufuatilia wala kuulizia malipo, wametuma ujumbe toka halmashauri kwa walimu wakuu kuwa tusiende kufuatilia mshahara wa mwezi wa nne hadi hapo itakapotangazwa, jaribu kufikiria tunaishi vipi ugenini?," alisema mmoja wa walimu hao.
Aidha mmoja wa walimu hao alisema hali ya maisha walipopelekwa ni ngumu ilhali wakitakiwa kununua vitu vya msingi vya kuanzia maisha kama vile godoro, kitanda, vyombo vidogo vya ndani na vinginevyo jambo ambalo wengine walifanya na kuishiwa kabisa na fedha kidunju waliopewa.
"Ndugu mwandishi hebu wewe fikiria unawezaje kuishi ugenini kwa shilingi 140,000/- hujanunua godoro, kitanda na maji ndoo moja huku tunanunua shilingi 500, vyombo vya ndani huna unaishi vipi katika hali kama hii?," alisema mmoja wa walimu hao huku akionesha kusikitika.
No comments:
Post a Comment