ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), Mhandisi William Mhando, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam, kuwa mshitakiwa wa pili (Eva Mhando) katika kesi ya matumizi
mabaya ya madaraka, si mke wake.
Mhandisi Mhando alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu
Mkazi, Frank Moshi, alipokuwa akisomewa maelezo ya awali katika kesi hiyo na
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Mhando alikiri maelezo kuwa alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Tanesco tangu Juni 2010 hadi 2012, lakini alikana maelezo kuwa mshitakiwa wa
pili (Eva Stephen Mhando) ni mkewe ambaye pia ni
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya
Santa Clara Supply Limited.
Kwa upande wake, Eva
alikubali kwamba aliwahi kuajiriwa na Tanesco kuanzia mwaka 1982 hadi 2009,
mshitakiwa wa tatu, France Mchalenge pia alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa
shirika hilo, wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na alikuwa
mjumbe wa Kamati ya Tathimini ya Zabuni namba Pa/001/11/HQ/G/011 ya vifaa vya
ofisi, ikiwemo printa na kompyuta.
Swai alidai mshitakiwa wa nne, Sophia Misidai aliajiriwa na
Tanesco na wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na mjumbe wa kamati
iliyofanya tathimini ya zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi katika shirika
hilo. Mshitakiwa alikubaliana na maelezo hayo.
Mshitakiwa wa tano, alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa
Tanesco na kuwa wakati wa uchunguzi alikuwa ofisa usambazaji na alikuwa mjumbe
wa kamati iliyotathimini zabuni hiyo.
Mheshimiwa Hakimu,
Kampuni ya Santa Clara Supply Ltd inamilikiwa na Eva Stephen William, Fred
William na Veronica Stephen Mhando, ilipata zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi
yenye thamani ya sh milioni 884.5.Mhando akiwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo
na Eva akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Santa Clara Supply Ltd alisaini barua ya kuipa
zabuni huku akijua wazi kwamba kampuni hiyo inamilikiwa na familia yake, pia
hakujitoa kuonyesha kwamba ana maslahi na kampuni hiyoalidai.
Wakili Swai aliendelea kueleza kuwa Mhando aliwapa zabuni
hiyo mshitakwa wa pili, Eva na watoto wake kinyume na utaratibu, walitaka
kuiuza kampuni hiyo kwa mtu mwingine wakati tayari walishapata zabuni ya
kusambaza vifaa hivyo vya ofisi, mshitakiwa wa kwanza (Mhando) alitumia
madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuonyesha kwamba ana maslahi binafsi na
Kampuni ya Santa Clara,” alidai Swai.
Swai alidai kwamba Eva alighushi taarifa za ukaguzi wa
hesabu za Kampuni ya Santa Clara ya mwaka 2007/2008 akionyesha kuwa Kampuni ya
Finx Capital House ilifanya ukaguzi.
Pia mshitakiwa huyo alighushi taarifa ya kuhamisha hisa
akionyesha hisa 200 zenye thamani ya sh 10,000 zilihamishiwa kwa Eveta
Shing’oma.
Eva alidaiwa kutoa taarifa ya ukaguzi wa fedha kwa Katibu wa
Bodi ya Zabuni wa Tanesco akionyesha zilifanyiwa ukaguzi Desemba, mwaka 2010,
akajipatia sh milioni 37.7 kutoka kwa shirika hilo.
Swai alidai Mchalange, Misidai na Naftali Kisinga walitoa
taarifa katika Bodi ya Zabuni kuonyesha kwamba Kampuni ya Santa Clara walikuwa
wana sifa ya kupata zabuni hiyo, walipata mkataba wa kusambaza vifaa vya
ofisini wenye thamani ya sh 884,550,000. Washitakiwa hao walikana maeneo yote
hayo.
Wakili Swai alieleza upande wa jamhuri unatarajia kuleta
mashahidi 14 na wanawasilisha mahakamani vielelezo 18.
Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 29-30, mwaka
huu, itakapokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
No comments:
Post a Comment