Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na
wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya
apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo
zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo
huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupakaDaktari wa Manispaa
ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na
vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi
kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.
"Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine
hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya
estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids," anasema.
Dk Chipata anasema kukua kwa
uvimbe kwenye kizazi hutokea
katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.
Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha
wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia
na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.
"Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe
kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya
ngozi kama vile mercury na hydroquionone," anasema.
Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za
vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au
kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).
"Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi
baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye
ngozi kutokana na mfumo wa ngozi," anasema.
Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi
kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi
kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye
kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium
na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na
wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani
ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo
kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na
wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi
hujulikana kama fibroids au myoma.Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi
wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza
kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo
kichwani kwa kipindi gani.
Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha
nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa
na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa
upasuaji.
Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za nywele hasa
zilizoandikwa "Lye Relaxer" ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa
yaliyoandikwa "No Lye Relaxer" yana calcium hydroxide na guanidine
carbonate.
Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa 'no lye relaxer'
zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile
zilizoandikwa "Lye Relaxer".
Uvimbe kwenye kizazi ni nini?
Ukuta wa nyumba ya uzazi umejengwa kwa misuli ya tishu. Kwa
kawaida uvimbe huu huanza kidogo kidogo na hukua hadi kufikia ukubwa wa tikiti
maji. Fibroids kubwa huweza kukua na kutanua nyumba ya uzazi na kuwa sawa na
ujauzito wa miezi sita au saba.
Mwanamke huweza kuwa na uvimbe mmoja mkubwa au vivimbe vingi
ndani ya kizazi.
Daktari Bigwa wa magonjwa ya uzazi wa Kitengo cha Upasuaji
cha Chuo Kikuu Sayansi ya Tiba Muhimbili, Henry Mwakyoma anauelezea fibroids ni
uvimbe ambao upo katika umbile la misuli myembamba na laini linalokua siku hadi
siku.
"Sababu inayopewa kipaumbele zaidi ni wingi wa
vichocheo vya estrogen ambavyo vipo katika miili ya wanawake," anasema.
Dk Mwakyoma anafafanua kuwa, vichocheo hivi ndivyo hufanya
kazi katika mwili wa mwanamke na kumsababishia kupata siku zake za hedhi.
"Ndiyo maana wengi wanaopata uvimbe huu, huwa ni
wanawake walio katika umri mkubwa au ambao tayari wamevunja ungo, kwani ndiyo
ambao huzalisha vichocheo vya estrogeni," anabainisha mtaalamu
huyo."Dalili hutegemeana na eneo ulipokaa uvimbe na ukubwa wake. Wengi
hugundulika wakati wa kujifungua au endapo mwanamke atapata uvimbe katikati ya
kizazi, basi huweza kutokwa damu kwa wingi," anasema.
Anaongeza: "Hata hivyo, asilimia 35 hadi 50 ya wanawake
wanaougua maradhi haya huonyesha dalili wakati wa kujifungua,"
Dalili nyingine ni mwanamke kutokwa damu zake za hedhi kwa
wingi na kwa siku nyingi. Damu za hedhi huweza kuwa nyingi au kidogo sana
zikiambatana na maumivu makali.
Anasema wakati mwingine mwanamke huweza kuhisi ana ujauzito
kwani uvimbe huu huwa mkubwa na huchezacheza kana kwamba ni kiumbe.
"Nina mifano hai, wapo wanawake waliowahi kuhisi wana
ujauzito, wakakosa kabisa siku zao za hedhi, wakaona dalili zote za mimba na
kumbe walikuwa na uvimbe wa fibroids," anasema.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema wamekuwa
wakifanya ukaguzi mara kwa mara kuzuia uuzwaji wake.
Isitoshe akasema: "Elimu inatolewa kwa wananchi pia ili
kuwafahamisha kuhusu madhara ya vipodozi hivyo kwa sababu wanunuzi wasipokuwepo
basi hata biashara haitakuwepo."
Pamoja na hayo, adhabu hutolewa ya kuwanyang'anya na
kuwapeleka mahakamani wenye maduka makubwa wakiziuza.CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment