Picha na Maktaba |
MBUNGE wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM), ambaye
pia ni Waziri wa Ulinzi wa zamani, jana alijikuta katika wakati mgumu wa
kuumbuliwa na mbunge mwenzake wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), wakati wawili hao
wakibishania uuzwaji tata wa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA).Hatua hiyo
ilijitokeza wakati Mtemvu akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na
Uchumi kwa mwaka wa fedha 2014/2015, na kuungana na wabunge wenzake kadhaa
waliotangulia kuchangia, akidai UDA imeuzwa kifisadi bila wabunge wa Mkoa wa
Dar es Salaam kushirikishwa.
Wakati Mtemvu
akiendelea kujenga hoja yake, Prof. Kapuya aliomba kumpa taarifa, akimweleza
kuwa mbunge kujishughulisha na uwekezaji si dhambi na kwamba UDA imeuzwa
kihalali wala hakuna ufisadi kama inavyodaiwa, isipokuwa mbunge huyo anatumika
kuwashawishi wabunge kupinga suala hilo. Baada ya Prof. Kapuya kuketi,
Mtemvu
aliendelea kuchangia akidai kuwa haipokei taarifa ya mbunge mwenzake kwa sababu
yeye ni miongoni mwa walioshirikia kuiuza UDA kifisadi akitumia nafasi yake ya
uwaziri.
“Yaani mtu mzima unasimama hapa unasema kwamba UDA iliuzwa
kihalali wakati wewe ulitumia nafasi yako ya uwaziri kushiriki ufisadi huo?”
Alihoji Mtemvu na kuongeza kuwa yeye hatumiki bali Prof. Kapuya ndiye
anazunguka hotelini Dodoma kuwashawishi wabunge watetee uuzwaji wa UDA na
kutamba kuwa video kamera zipo zikimuonyesha akifanya hivyo.
Wakati Mtemvu
akieleza hivyo, wabunge wengi walimshangilia kwa nguvu, hususani wale wa kutoka
Mkoa wa Dar es Salaam, ingawa Naibu Spika, Job Ndugai, aliingilia kati na
kumtaka ajielekeze kwenye hoja badala ya kuendeleza mashambulizi binafsi.
Mkulo afunguka
Waziri wa Fedha na
Uchumi wa zamani, Mustafa Mkulo amevunja ukimya na kutoa siri ya uuzaji wa
kiwanja cha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC). Kiwanja hicho ambacho
Mkulo alidaiwa kukiuza kifisadi ni kile kilichopo Barabara ya Nyerere, jijini
Dar es Salaam.
Akijibu tuhuma hizo kwa mara ya kwanza, Mkulo alisema
kiwanja hicho kimeuzwa kama ilivyouzwa UDA ambayo hadi sasa ipo kwenye mzozo
mkubwa unaoligawa Bunge.
Alisema yeye wala wizara yake, hawakuhusika na uuzwaji wa
kiwanja hicho ambacho kwa mara ya kwanza alitajwa bungeni kuwa mhusika mkuu na
mwizi namba moja. Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa
mwaka wa fedha 2014/2015, Mkulo alisema waliohusika na uuzwaji wa kiwanja hicho
ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, Prof. Khamis Mahigi na aliyekuwa Mkurugenzi
wa shirika hilo, Methusela Mbanjo.
“Aprili mwaka 2012,
nilituhumiwa kuuza kiwanja hicho, leo nataka kutoa ufafanuzi kwa sababu
nimepata nafasi, mimi sikuuza wala sikushiriki mchakato wa kuuza kiwanja. “Bodi
ya CHC iliandikia Wizara ya Fedha barua ya kuomba kibali cha kuuza kiwanja
chao, barua hiyo haikwenda wizarani isipokuwa ilikwenda kwa Msajili wa Hazina,
ambaye baada ya uchambuzi wa kina akatoa ushauri kwa Katibu Mkuu naye akatoa
mapendekezo yake kwa Waziri wa Fedha nini kifanyike.
“Mapendekezo ya
msajili yalionyesha udhaifu kwenye maombi ya CHC ambapo baada ya kuona upungufu
huo, nikiwa waziri nikaagiza bodi ifuate taratibu, kanuni na sheria kisha ilete
upya kwa sababu hiyo ni mali ya serikali. “Baada ya siku chache wizara ikapata
taarifa kwamba CHC ilikuwa imeshapokea nusu ya gharama ya mauzo ya kiwanja
kile, kwa maana kwamba bodi ilikuwa imeshauza kiwanja na barua kwamba waziri
atoe kibali ilikuwa ni geresha,” alisema Mkulo ambaye ni mbunge wa Kilosa
(CCM).
Mkulo alisema
kuthibitisha kwamba hakuhusika na uuzwaji wa kiwanja hicho, mkataba wake
ulisainiwa miezi mitano baada ya yeye kuondoka hazina. Alisema karatasi na
nyaraka zote zilizotumwa kwenye magazeti zilikuwa feki, lakini zilitoka CHC.
Mkulo alisema wabunge waliomlipua bungeni walikuwa wakipita
na nyaraka hizo huku wakimtuhumu kuwa yeye ni mwizi namba moja.“Kiwanja hiki
kiliuzwa na wenyewe kama ilivyouzwa UDA, ila hii ni mbaya zaidi ya UDA.
“Nikisema niyaseme
yote hapa wabunge wenzangu mtatapika, wakati ule yanatokea bungeni mimi
nilikuwa Washington DC kwenye mkutano wa Benki ya Dunia, niliomba nafasi kutoa
utetezi wangu humu bungeni, lakini kwa bahati mbaya sikupata hadi nilipoondoka
Hazina,” alisema.
Mkulo alisema kuwa
aliona ayaseme hayo jana kwani yeye ni Muislamu, marehemu baba yake alikuwa
sheikh na babu yake alikuwa chifu, na hivyo anataka afe kwa heshima kwa kusema
ukweli.
No comments:
Post a Comment