Divorc Origi ni mkenya na mwanaafrika mashariki wa kwanza
kushiriki kombe la dunia
Mshambuliaji wa Lille ya Ufaransa , Mkenya Divorc Origi
ambaye ni mzaliwa wa Ubelgiji ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ambayo
imeondoka Jumanne kuelekea Brazil kwa mashindano ya kombe la dunia kuanzia
Alhamisi wiki hii.
Origi, mwanae Mike Okoth, mchezaji wa zamani wa timu ya
taifa ya Kenya Harambee Stars atakua mchezaji wa kwanza wa Afrika Mashariki
kuiwakilisha Ubelgiji, na yuko pamoja na wachezaji nyota kama vile Vincent
Kompany wa Manchester City na Eden Hazard wa Chelsea.
Watakabiliana na Algeria mechi yao ya kwanza ya kundi H Juni
tarehe 17 na siku tano baadae wanapepetana na Urusi kisha Korea Kusini kwenye
mechi za mchujo.
Akizungumza na BBC kwa njia ya simu akiwa Ubelgiji Origi
anasema:'' Algeria ni timu yenye wachezaji wazuri kwa hivyo hatuwezi kuidharau.
Tutacheza mchezo wetu wa kawaida lakini nina matumaini makubwa tutashinda.’’
Anasema Urusi na Korea pia si timu hafifu hasa Warusi. Lengo lake kubwa ni
Ubelgiji kufuzu kwa raundi ya pili kisha kutoka hapo anasema mambo yatakuwa
sawa kabisa.
Kuhusu mbona ameamua kuiwakilisha Ubelgiji na sio taifa la
babake Kenya, Origi anasema alitilia maanani mambo mengi kama vile usimamizi
mzuri wa kandanda nchini humo, mizizi yake ya kandanda iliyoko huko, marafiki,
ushauri wa babake pamoja na Ubelgiji kufuzu kwa kombe la dunia kwani
haijulikani ni mwaka upi Kenya itafuzu kwa kombe la dunia.
Tukiwa tunazungumzia hilo babake Origi, Mike Okoth, naye
anajitupa uwanjani kwa kusema:''Mimi nilimshauri aichezee Ubelgiji na sio Kenya
kwa sababu kusema kweli kama angechezea Harambee Stars kuna mambo ambayo
hangestahimili hasa usimamizi mbovu. Mimi nilivumilia kwa saababu nimezaliwa
Kenya lakini mwanangu hangeweza kabisa. Na tena bado ni mchanga kwa hivyo ni
vyema aiwakilishe Belgium. Nakumbuka siku moja tukiwa na Harambee Stars
tulilala kwenye jumba moja ambalo bado lilikua linajengwa huko Afrika
Magharibi.’’
Namuuliza Okoth kama kuna siku Harambee Stars itafuzu kwa
kombe la dunia? ''Itakua vigumu sana kwao kufuzu kwa kombe la dunia kama
usimamizi ni duni bado,’’ anasema Okoth, na kuongezea:''Tena wanahitaji wawe
wakicheza na timu mashuhuri duniani mara kwa mara. Sio kwamba ni vigumu kufuzu
lakini lazima pia serikali nayo ikubali kutumia fedha kulipia mechi kubwa za
kimataifa na tuwe na msingi mzuri wa kandanda kuanzia mashinani.’’
Origi, mwenye umri wa miaka 19, anasema amefurahia sana
kuchaguliwa kuiwakilisha Ubelgiji kwenye kombe la dunia, na vile vile kuwa na
mshambuliaji mahiri Romelu Lukaku wa Chelsea ambaye msimu uliopita alichezea
Everton kwa mkopo.
''Wachezaji wote wananipa morali sana. Rafiki yangu Hazard
(Eden) na Kompany (Vincent) wameniambia nicheze mchezo wangu wa kawaida nisiwe
na wasiwasi uwanjani,’’ asema Origi aliyecheza mechi ya mwisho ya kirafiki
dhidi ya Tunisia ambayo Ubelgiji ilishinda kwa bao 1-0. Namuuliza kama ananuia
kuhamia England lakini Origi anasema kwa sasa mawazo yake yote yako Brazil kwa
kombe la dunia. Babake Origi ni shabiki mkubwa wa Liverpool.
Mara ya mwisho Ubelgiji kushiriki kombe la dunia ni mwaka wa
2002 ambapo kocha wao wa sasa Marc Wilmots alikuwa mchezaji wa mwisho kuifungia
Ubelgiji kwenye kombe la dunia hadi sasa. Wilmots ana imani na Origi ambaye
amechukua nafasi ya Christian Benteke wa Aston Villa anayeuguza jeraha.
Urusi ndio tisho kubwa kwa Ubelgiji kumaliza katika nafasi
ya kwanza kundi H, na ina motisha wa kufanya vyema kwani wao ndio wataanda
kombe la dunia mwaka wa 2018. Isitoshe Urusi inafunzwa na kocha anayeaminika
kulipwa mashahara wa juu zaidi duniani Fabio Capello ambaye anaweka kibindoni
dola millioni 6.5 kwa mwaka. Matokeo mazuri zaidi kwa Urusi kwenye kombe la
dunia ni mwaka wa 1966 walipomaliza wa nne.
No comments:
Post a Comment