Mwananchi huyu alikutwa akiuchuna mzoga wa punda huyu huko
Migori wilayani Iringa. Maeneo mengi ya vijijini katika Mkoa wa Iringa
yanalalamikiwa na wananchi kwamba wanalishwa mizoga ya punda, paka na mbwa.
(Picha na Said Ng’amilo).
Na Mathias Canal, Iringa
WAKAZI wa Kitongoji cha Lugofu katika Kijiji cha Ilandutwa,
Wilaya ya Iringa Vijijini, mkoani Iringa wamelaani kitendo cha baadhi ya
wafanya biashara wa nyama kijijini hapo kuwalisha nyama ya paka, mbwa na punda
pasipo kujua.Wakizungumza na Kwanza Jamii kijijini hapo, wanakijiji hao
walisema mara ya kwanza walipopata taarifa ya kulishwa nyama ya paka hawakutoa
taarifa kwa mtu yeyote kutokana na kuamini kwamba wafanyabiashara hao
watajirekebisha kwa kuacha uuzaji wa nyama hizo haramu.
Hata hivyo, vitendo hivyo vimeendelea kushika kasi ambapo
wafanyabiashara hao wamekuwa wakiokota hata mizoga ya punda, paka na mbwa
waliogongwa na magari au kukamata mbwa wa watu kijijini hapo na kuiuza nyama
hiyo kwa wananchi kinyume cha sheria na taratibu za afya.
Vincent Mtale mkazi wa Kitongoji cha Lugolole “A” amesema
Balozi wa Kitongoji cha Lugofu, Ngojea Ng’alla, hivi karibuni aliiba mbwa wa
Angelina Kanyika na kumpeleka kwa kijana anayefahamika kwa jina la Manati
Dunda.“Mtu mmoja anayeitwa Nung’uniko alimfukua punda aliyekufa akazikwa, hivyo
yeye akamchuna na kutengeneza supu ya mchanganyiko wa nyama ya punda, nyama ya
nguruwe na viazi mviringo na kuiuza kwenye kijiji hicho ambacho nyama hiyo
ilishambuliwa kwa kasi na wanakijiji bila wao kufahamu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lugolole “A” amekiri kuibiwa kwa
mbwa wa mama huyo na kuuzwa Shs. 12,000 kwa makubaliano ya kuchanganya na nyama
ya nguruwe na viazi ili watu wasitambue kama kuna mchanganyiko huo ili waweze
kugawana fedha zitakazopatikana baada ya mauzo.Angelina Kanyika mwenyewe
amewataja vijana wawili waliohusika na wizi huo wa mbwa wake aliyekuwa na
mimba, kuwa ni Ngojea Ng’alla na mwenzake Manati Dunda ambapo baada ya
kumchinja wakawatupa watoto waliokuwa tumboni.“Baada ya kufanya upelelezi juu
wa mbwa wangu niligundua watu hao ndio waliokwiba, nimesikitishwa sana kwa
kitendo hicho kwani mbwa wangu aliuawa kwa kupigwa marungu hadi kufa kabla ya
kumchuna,” alisema kwa masikitiko.
Hata hivyo, Dunda amekiri kuiba mbwa, kuchinja na kuuza
vibudu kijijini hapo na kwamba amekuwa akifanya hivyo kwa miaka mitano sasa.Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilandutwa, Isack Nganingo, amekiri kuuzwa
kwa nyama hizo haramu kijijini hapo huku akikiri kuibwa na kuchinjwa kwa mbwa
wa Angelina Kanyika na hatimaye nyama yake kuuzwa katika kijiji hicho.Mwenyekiti
huyo ametoa rai kwa wananchi wanaotaka kuchinja mnyama wa aina yeyote kijijini
hapo kufika ofisini kwake ili kupewa kibali cha kuchinja mnyama huyo kwa
kuzingatia taratibu na kanuni za afya.
No comments:
Post a Comment