Saa nne unusu jioni Jumapili, Ufaransa ilikuwa inacheza
dhidi ya Honduras katika mojawapo ya mechi za kombe la dunia.Lakini mechi
ilipokuwa inaendelea,katika eneo la Mpeketoni mauaji ya kinyama yalikuwa
yakifanyika.Ujumbe kutoka kwa afisa mmoja wa shirika la msalaba mwekundu
ulikuwa na ishara zote za mashambulizi ya kigaidi sawa na kile ambacho wengi
wamekuwa wakishuhudia katika mbinu ya mashambulizi inayotumika na Boko Haram
nchini Nigeria.
''Milio mikubwa ya risasi inasisika katika eneo la
Mpeketoni, katika jimbo la Lamu. Mashambulizi yamekuwa yakiendelea kwa saa moja
sasa. Kituo cha petroli kimeteketezwa na hoteli kushambiliwa.Tunasubiri taarifa
zaidi,'' alisema afisaa huyo wa shirika la Red Cross.Usiku wa kuogofya wenye
mashambulizi ambayo yalidumu kwa muda wa saa kumi. Walioshuhudia walisema
waliona zaidi ya watu 50 wakiwa wamejihami vikali na kuanza kufanya msako ndani
ya nyumba za watu.
Magari mawili yaliyokuwa yameibwa ndiyo yaliyotumika
kuwabeba washambulizi hadi katika eneo la Mpeketoni umbali wa kilomita 40
kutoka ufuo wa bahari hindi.Mashambulizi hayakuharakishwa. Washambuliaji
walisemekana kuongea Kisomali na kiswahili huku wakibeba bendera ya Al Shabaab
na kutamka 'Allahu Akbar'', yaani Mungu ni mkubwa.
'Kwa nini Mpeketoni? '
Eneo hilo ambalo halina ulinzi mkali bila shaka lilikuwa
sehemu ya karibu sana kwa Al Shabaab kushambulia. Linakaribiana na Somalia.
Kundi hilo halikusita kukikri kutekeleza mashambulizi hayo, saa 24 baadaye.
Walioshuhudia walisimulia visa vya kuogofya wakati
washambuliaji walipokuwa wanaendesha mashambulizi nyumba hadi nyumba wakimuua
kila mwanamume waliyemuona.
Wanawake na watoto walisazwa. Mashambulizi yalifanya kwa
masaa kadhaa kabla ya polisi kuchukua hatua.Mfumo wa mashambulizi na ukubwa wa
mashambulizi yenyewe umewaacha wengi wakiwa na maswali si haba. Kwa nini
Mpeketoni? Na kwa nini wanaume pekee ndio waliouwa?
Al Shabaab walituhumiwa kwa mauaji ya wanawake na watoto
katika shambulizi la awali dhidi ya jengo la kifahari la Westgate mwaka jana
mjini Nairobi.Mashambulizi ya kiholela ambayo pia yaliwalenga waisilamu,
yaliwaghadhabisha wale ambao huunga mkono kundi hilo.
'Al Shabaab wabadili mbinu'
Al Shabaab sasa wameamua kubadili mbinu wanaotumia
kushambulia kwa hofu ya kupoteza uungwaji mkono.Shambulizi la Mpeketoni,
ilikuwa njia mojawapo ya kusafi sifa yao. Kuua wanaume na kuwasaza wanawake na
watoto.
Mpeketoni ni eneo lenye rotuba nzuri ya kufanyia kilimo wala
sio eneo ambalo ni kivutio kwa watalii. Maafisa wa usalama huenda walikutwa
ghafla bila ya kujiandaa kukabiliana na shambulizi la aina yoyote.
Katika siku za nyuma, makundi ya kigaidi yamekuwa yakilenga
miji mikubwa ya Kenya kwa mashambulizi lakini sasa inaonekana kuwa kundi hilo
limeanza kubadili mbinu ya mashambulizi na kuanza kulenga vijiji.Serikali ya
Kenya imelaumu uchochezi wa kisiasa kwa mashambulizi hayo na kuwaonya wanasiasa
dhidi ya kuchochea ghasia na matamshi ya chuki miongoni mwa wananchi.
Kuna mjadala mkali kuhusu nani aliyetekeleza mashambulizi
hayo. Baadhi wanahisi kuwa licha ya kwamba Al Shabaab wamekiri kuyatekeleza,
sio wao , serikali ya Kenya imesema wazi kuwa yalichochewa kisiasa.CHANZOBBC
No comments:
Post a Comment