BAADA ya Simba kumkosa kipa wa Yanga, Ally Mustapha
‘Barthez’ ambaye amesaini mkataba mpya na timu yake, kocha wa makipa wa
Msimbazi, Iddi Pazi, amesema hakuna jinsi, haraka sana Juma Kaseja anatakiwa
kurudi Simba ili acheze kwa raha.
Kabla ya Yanga kumsainisha Barthez, Simba ilikuwa imepiga
hesabu za kumrudisha kipa wao huyo wa zamani ili apambane na Ivo Mapunda ambaye
hana mpinzani katika kikosi cha timu hiyo.
Kocha huyo alisema,
kuna sababu tatu zinazomfanya Kaseja
kuondoka Yanga kwani akibaki hatoweza kufanya kazi yake kwa furaha na
mafanikio.
Alisema kwanza ushindani wa nafasi kati yake na makipa Deo
Munishi ‘Dida’ na Barthez ni mkubwa. Pili anaonekana hakubaliki kwa mashabiki
wa Yanga na tatu ni ujio wa kocha Marcio Maximo katika kikosi hicho.
Pazi alisema: “Mahali alipo Kaseja (Yanga), kunaweza
kumfanya astaafu kabla ya muda wake au hata kuendelea kucheza soka kwa mashaka
hivyo namtaka afikirie kurudi Simba ili kutunza heshima na kufanya kazi yake
kama ilivyokuwa awali.
“Kaseja si kipenzi cha mashabiki Yanga na inapokuja wakati
wa kazi anaweza kupata wakati mgumu kutokana na kuzomewa na kumfanya
kutojiamini akiwa kwenye kazi yake.
“Pia nimesikia Yanga wanamleta Maximo, nafikiri ni hofu kwa
Kaseja kwa sababu siku za nyuma kocha huyo alitofautiana naye wakiwa Taifa
Stars, aje Simba ili awe na amani.”
Pazi pia amemtaka kipa huyo kufuta ndoto za kustaafu soka wakati
huu ili awe kocha akisema kipa huyo bado ana uwezo wa kucheza.
“Nafikiri wapenzi wa Simba wanatakiwa kumpa Kaseja nafasi
kwenye mioyo yao. Amefanya mengi na naamini akirudi ataweza kufanya mengi na
kumalizia soka lake Simba akiwa na heshima,” alisisitiza.
CHANZO: MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment