Kiungo wa Italia Riccardo Montolivo atalikosa Kombe la Dunia baada ya kuvunjika mguu wakati wa mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliomalizika kwa sare ya 0-0 dhidi ya Jamhuri ya Ireland katika dimba la Craven Cottage.
Mchezaji huyo wa AC Milan, 29, aliondolewa uwanjani na machela baada ya kukumbana na mlinzi wa Reading Alex Pearce.
Daktari wa timu ya Italia Enrico Castellacci amesema: "Sijaona picha ya X-ray ili kuelezea jambo hili, lakini kwa mfupa uliovunjika unaweza kutegemea upasuaji."
Italia watakutana na England, Uruguay na Costa Rica kwenye Kundi D.
Montolivo, aliichezea Italia mchezo wa 58 kwa dakika nane kwenye mchezo wa kirafiki kujiandaa na fainali za Kombe la Dunia, lakini aliondolewa uwanjani akiwa juu ya machela na kuwahishwa katika hospitali moja mjini London kwa ajili ya X-rays, ambayo ilithibitisha uharibifu huo kwenye mguu wake.
Nafasi yake ilichukuliwa na kiungo wa zamani wa Liverpool Alberto Aquilani, ambaye hakurudi tena dimbani baada ya mapumziko akidai kutojisikia sawa.
Mchezaji mwenza wa Aquilani katika klabu ya Fiorentina Giuseppe Rossi anaweza kujihakikishia nafasi katika kikosi cha Italia kitakachokuwa na wachezaji 23 kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, licha ya kucheza kwa dakika 70 akirejea kutokana na maumivu ya goti.
No comments:
Post a Comment