Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, June 12, 2014

Mahakama yaelezwa bilionea wa madini alivyouawa

Na Daniel Mjema, Mwananchi
Mawakili wa Serikali watumia saa saba kusoma ushahidi, kesi sasa yahamia Mahakama Kuu.
Moshi. Bunduki ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) iliyotumika kumuua mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya, ilinunuliwa kwa Sh4 milioni nchini Kenya, Mahakama imeelezwa.
Imeelezwa pia kwamba wauaji wanne waliokwenda eneo la tukio kutekeleza mauaji hayo, walilipwa Sh5 milioni kila mmoja na washirika wao wakilipwa Sh3 milioni kila mmoja.
Hayo yamo katika maelezo ya mashahidi 57 kwa washtakiwa yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro, Munga Sabuni juzi na mawakili wa Serikali, Stella Majaliwa na Florentina Sumari waliokuwa wakipokezana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
 
Msuya aliyekuwa anamiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kumiminiwa risasi Agosti 7, mwaka jana saa 6:30 mchana Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro na katika maelezo yake, mtaalamu aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Dk Paulo Christopher alisema ulikuwa na matundu 26 ya risasi yaliyotokana na risasi 13 zilizoingia na kutokea upande wa pili zikichanachana utumbo, mapafu, ubongo na bandama.
Ushahidi huo unadai kuwa katika eneo la tukio, polisi waliokota maganda 22 ya risasi za SMG.
Mtaalamu wa makosa ya kijinai ya kompyuta, Koplo William Obeid alieleza kuwa katika kufanikisha mauaji hayo, laini mpya tano za Airtel zilisajiliwa kienyeji, zote zikiwa na jina la Motiti Ndoole na laini iliyotumika kumvuta marehemu eneo la tukio ilikuwa 0682405323.
Katika ushahidi huo, Inspekta Samwel Maimu alidai kuwa washtakiwa walikiri kosa na kueleza kuwa bunduki aina ya SMG ilinunuliwa Namanga, upande wa Kenya. Inspekta Maimu alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed ndiye aliyetoa Sh4 milioni za kununua silaha hiyo na kutoa fedha za kusajili line mpya tano za simu.
Pia alidai kuwa mshtakiwa huyo, ndiye aliyetoa Sh3,350,000 zilizotumika kununulia pikipiki mbili moja aina ya Toyo na nyingine King Lion zilizotumiwa na wauaji siku ya tukio.
Katika maelezo hayo yaliyosomwa mahakamani, mshtakiwa wa kwanza (Shariff), anadaiwa kueleza namna alivyotoa maagizo ya kusajiliwa kwa line mpya.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa mshtakiwa wa saba, Ally Mussa ndiye aliyemshauri atoe jiwe moja la Tanzanite litakalotumika kumshawishi marehemu Msuya. Katika maelezo hayo, ilidaiwa kuwa ndiye aliyelipa Sh4 milioni za kununua bunduki hiyo ya SMG na kwamba siku ya tukio aliibeba kwa gari lake hadi eneo la tukio na kuwakabidhi wauaji.
Katika ushahidi huo, mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa anadaiwa kueleza kuwa yeye ndiye aliyemmiminia risasi marehemu ambazo hajui idadi yake na kwamba bunduki hiyo aina ya SMG waliinunua Namanga na ilihifadhiwa nyumbani kwa Shariff sambamba na pikipiki zilizotumika.


Katika maelezo yake, mshtakiwa wa saba, Ally Mussa au Majeshi anadaiwa kueleza kuwa ndiye aliyepewa kipande cha madini na kwenda kumuuzia marehemu hotelini kwake SG Resort siku moja kabla ya mauaji.Mshtakiwa huyo anadaiwa kukiri kuwa siku hiyo alikwenda na vipande vitatu vya madini lakini akakataa kuuza vipande viwili akisema yuko na wenzake na kukubaliana kufanya biashara siku inayofuata na kwamba siku ya mauaji, yeye ndiye aliyemtumia ujumbe wa maandishi ya simu marehemu na kukutana naye na kwenda naye hadi eneo la mauaji.
Katika maelezo yake shahidi huyo anadaiwa kusema: “Tulipofika Mjohoroni, Erasto alishuka ili kukutana na Karimu, mimi nikabaki kwenye gari, ndipo Karim akatoa bunduki na kuanza kummiminia risasi Erasto.”
Alidai kuwa baada ya mauaji hayo, alipakia pikipiki aina ya Toyo iliyokuwa ikiendeshwa na Karimu aliyekuwa na bunduki hiyo ya SMG.
Mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne maarufu kama Mredii, anadaiwa kueleza kuwa Julai 26 mwaka jana, Shariff alimfuata na kumweleza kuwa kuna kazi ya kumuua Erasto.
“Nilimweleza siwezi kuifanya ila nitamtafutia vijana wa kufanya. Alinipa Sh300,000 na kunijazia mafuta ‘full tank’ niende kuwatafuta Ally Majeshi na Jalila,” ushahidi huo umedai.
Kesi hiyo, imehamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania na inasubiri kupangiwa Jaji.

No comments:

Post a Comment