Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam imesema itawachukulia hatua za kisheria wamiliki wa klabu za
usiku zinazokiuka maadili kwa kuruhusu klabu zao kupiga ngoma ya
‘bunyerobunyero’.
Ngoma hiyo iliibuka na
kuwa maarufu hasa jijini Dar es Salaam baada ya Polisi kupiga marufuku ngoma ya
‘kantangaze-kigodoro’ na ‘khanga moko’.
Onyo hilo lilitolewa
jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova wakati
akizungumza na waandishi wa habari. Alisema ngoma hiyo imeibuka karibuni
na inaenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Alisema ngoma hizo hazina
tofauti kubwa na vigodoro isipokuwa wahusika wa ‘bunyerobunyero wametofautisha
maeneo ya kupinga ngoma hiyo ambayo ni kwenye klabu za usiku tofauti na
vigodoro ilikuwa ikipigwa mitaani.
“Tutahakikisha kwa kushirikiana
na halmashauri za miji pamoja na polisi kuhakikisha hizi ngoma za
‘bunyerobunyero’ tunazipiga marufuku, kwasababu zinakiuka maadili,” alisema
Kova.
Alisema Polisi imetoa
onyo mara nyingi kuhusu ngoma hizo na kwamba hatua inayofuata sasa ni kuwakamata
wachezaji na wahudhuriaji wa ngoma hizo pamoja na kuwakamata wamiliki wa klabu
hizo na kuwapiga faini na kuzifungia klabu hizo.
“Onyo hili linatolewa
kwasababu hizi ngoma zimeenea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam,” alisema.
Kamanda Kova alisema
ngoma hizo zimetawaliwa na udhalilishaji wa hali ya juu jambo linalochangia
kuporomoka kwa maadili, hivyo hawatalifumbia macho.
“Uchunguzi kwasasa
unafanyika na endapo itabainika ngoma hizo kuendelea kuchezwa basi Jeshi la
Polisi na halmashauri za miji zitachukua hatua mbalimbali za kisheria ikiwa ni
pamoja na kuzifungia klabu hizo kwasababu zinakiuka taratibu za leseni,”
alisema.
No comments:
Post a Comment