Polisi wanachunguza ikiwa mtoto huyo alianguka kutoka kwa
ndege au la
Shughuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo
Kenyatta zilisitishwa kwa muda Jumatano asubuhi baada ya mwili wa kijana mdogo
kupatikana karibu na eneo la kurukia ndege
Mkuu wa kitengo cha Polisi katika uwanja huo, kamanda,
Joseph ole Tito, amesema kuwa mwili huo ulipatikana katika sehemu ya kurukia
ndege ,Hata hivyo alisisitiza kuwa ndege zilizokuwa zinaingia uwanjani humo
asubuhi na mapema hazikuathiriwa na tukio hilo.
Halmashauri ya huduma za ndege ilisema kuwa uwanja ulifungwa
kwa dakika arobaini baada ya maafisa wa usalama kugundua mwili huo.Kwa mujibu
wa maafisa hao, hatua ya kufunga uwanja huo ilifanywa ili kuondoa mwili wa
kijana huyo.Ni ndege ya shirika la ndege la Uturuki tu ndiyo ililazimika
kusalia angani kwa muda huku mwili wa kijana huyo ukiondolewa uwanjani.Kijana
huyo anaaminika kuwa na kati ya umri wa miaka 10 na 12 na alikuwa na majeraha
upande wa kushoto wa mwili wake.
''Mwili wake uliondolewa katika eneo hilo na kwamba
uchunguzi unaendelea kufanywa,'' alisema bwana Tito.Polisi wamesema watafanya
uchunguzi kubaini ikiwa alianguka kutoka kwa gurudumu la ndege au mtoto huyo
alifariki kutokana na sababu nyinginezo.Pia miongoni mwa maswali yanayoulizwa
ni vipi mwili wake ulipatikana katika uwanja wa ndege hasa katika njia ya
kurukia ndege?
Visa vya watu kupanda kwenye magurudumu ya ndege kimagendo
kwa lengo la kusafiri kwenda nchi nyingine vimekuwa vikiripotiwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment