Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii imeagiza vyombo vya dola, kukamata waganga wa jadi,
wanaojitangaza kutibu magonjwa ya Ukimwi, kisukari na shinikizo la damu.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk
Seif Rashid alipokuwa akiwasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha
2014/15.
Aliwasihi
wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala, kuacha mara moja, kujitangaza kuwa na
uwezo wa kutoa tiba dhidi ya ugonjwa wowote ule ambao uwezo huo
haujathibitishwa kitaalamu.
Waziri
huyo alisema yapo matangazo yanayohusu kuwa na uwezo wa kutibu Ukimwi, kisukari
na shinikizo la damu. “Kwa mujibu wa Sheria ya Tiba asili na Tiba mbadala,
matangazo hayo yaondolewe mara moja,” alisema.
Alieleza
kuwa wizara itatoa mwongozo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili dawa husika
zithibitishwe kitaalamu.
“Napenda kuchukua fursa hii kuagiza vyombo
husika vya serikali, vifuatilie kwa karibu na kuchukua hatua kwa mujibu wa
sheriakwa wale watakaokwenda kinyume na sheria,” alisema.
Waziri
huyo pia alizungumzia suala la tiba za kibingwa, ili
kupunguza
idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kwa uchunguzi na matibabu.
Alisema
Wizara inaendelea kuanzisha huduma za tiba za kibingwa katika hospitali za
Kanda, hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kupunguzwa wagonjwa
hao wa kwenda nje ya nchi.
Alisema
huduma za upasuaji mkubwa wa moyo, zimeendelea kutolewa ambapo hadi sasa
wagonjwa 671 walipata huduma hiyo kwa mafanikio katika hospitali za Muhimbili,
Bungando na KCMC.
Aidha,
wagonjwa 211 walifanyiwa upasuaji maalum katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(MOI), ambapo 29 walifanyiwa upasuaji wa ubongo, 107 upasuaji wa uti wa mgongo, 56 waliwekewa
viungo bandia vya nyonga na 19 viungo bandia vya goti.
Dk
Rashid alisema katika mwaka 2014/15 Taasisi ya Mifupa Muhimbili
inatarajia kuwahudumia wagonjwa wapatao 6,900.
Aidha,
itafanya upasuaji wa kuweka viungo bandia vya nyonga kwa wagonjwa 400, kuweka
viungo bandia vya goti kwa wagonjwa 150, upasuaji wa ubongo kwa wagonjwa 240,
upasuaji wa uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kwa wagonjwa 400 na upasuaji wa
watoto wenye vichwa vikubwa 600.
Bajeti
aliyoomba ili kuiwezesha Wizara yake kutekelezwa kazi zilizopangwa katika mwaka
2014/15, Waziri huyo aliomba Bunge kuidhinisha makadirio ya
matumizi ya wizara hiyo pamoja na taasisi zake yenye Sh bilioni 622.95, ambapo
kati ya hizo Sh bilioni 317.22 ni kwa ajili ya matumizi ya kwaida na Sh bilioni
305.72 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment