Pages

Tuesday, June 10, 2014

Shemejiye Karume sasa ajiunga CUF




Aliyekuwa mwakilishi wa CCM wa jimbo la Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid, ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).



Himid aliyewahi kuwa Waziri mwandamizi chini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) chini ya Rais Ali Mohammed Shein na hapo kabla chini ya Rais Mstaafu wa Amani Karume, alifukuzwa uanachama wa CCM Agosti 26, mwaka jana kwa madai ya kukisaliti chama chake.



Himid anayedaiwa kuwa ni shemeji yake Rais Karume, baada ya kuweka bayana azma hiyo, alisema katika uchaguzi mkuu wa mwakani anakusudia kugombea kiti cha jimbo hilo kupitia CUF.



Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CUF mjini hapa mwishoni mwa wiki, alisema atawashauri vijana wampigie kura Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad,ili awe Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwakani.




“Mimi ni mpenzi wa Maalim Seif Sharif na kura yangu anayo na nitashirikiana na wezangu kuzitafuta kura za ziada ili awe Rais wa Zanzibar, “alisema Himid.



Alieleza kuwa bidhaa zikiwa nyingi sokoni mteja ana haki ya kuchagua iliyo bora, hivyo ana imani kuwa CUF ndilo kimbilio la Wazanzibari ili kuifanya nchi hiyo iwe na mamlaka kamili.



Alisema moja ya sababu ya kufukuzwa CCM ni kusema ukweli na kusimamia maridhiano ya wananchi kwa kutaka muundo wa serikali tatu na kusema Muungano uliopo wa serikali mbili hauna heshima kwa Wazanzibari na taifa lao.



“Mimi nisiwe kigeugeu, nasema kuwa Muungano huu hauna heshima hata kidogo, Zanzibar tunahitaji mamlaka kamili ili kujiendesha kiuchumi,” alisema Himid na kuongeza kuwa Muungano wa nchi na watu siyo mbaya, lakini muundo uliopo wa serikali mbili haufai kwani Zanzibar itaendelea kuwa mtumwa chini ya muundo huo.



Katika mkutano huo uliofanyika jimboni Mji Mkongwe na kuhudhuriwa na umati wa wafuasi ukiambatana na mbwembwe na nderemo hasa baada ya Himid kupanda jukwaani kwa mara ya kwanza kuwasalimia wananchi, uwanja ulisisimka kwa kupiga kelele za kauli mbiu ya CUF ‘ya haki sawa kwa wote.’



Mwanachama huyo mpya alidai kutimuliwa uanachama na Kamati Kuu ya CCM kumetokana na msimamo wake ambao chama hicho kilisema kuwa ulikwenda kinyume na sera na taratibu inazosimamia.



Kabla ya hatua hiyo alikuwa anatoa kauli mbalimbali za kutaka Zanzibar imiliki rasilimali zake hasa gesi na mafuta badala ya kuwa jambo la Muungano.



Aidha, alisimama kidete kutaka muundo wa Muungano wa mkataba ambao ulikuwa msimamo wa CUF, ingawa chama hicho hivi sasa kimejielekeza kutetea muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokusanya maoni chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.



Himid alikuwa mwakilishi wa jimbo la Kiembe Samaki kwa miaka minane ambapo alichaguliwa mwaka 2005 kwa kupata kura nyingi, lakini Agosti mwaka jana alifukuzwa CCM.



Kabla ya kufukuzwa uanachama alipata kuwa Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 na kuchaguliwa tena kuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili mwaka 2010 hadi 2013 alipoondoshwa kwenye nafasi hiyo kuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum kwa muda wa miezi mitatu hadi aliopofukuzwa CCM.



Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, katika mkutano huo alisema kiu ya Wazanzibar ni mamlaka kamili ya dola.Alisema maridhiano ya SUK hayakuwa tu kuwaunganisha Wazanzibari, lakini pia lengo lilikuwa kuyarejesha mamlaka kamili ya Zanzibar.



“Ingekuwa viongozi wote wa SUK wangeshirikiana mamlaka kamili ya Zanzibar ingepatikana,”alisema Jussa.



Alisema ili mamlaka kamili ya Zanzibar ipatikane ni mpaka Maalim Seif awe Rais wa Zanzibar na ana imani kuwa dawa ya hilo karibu litapatiwa ufumbuzi ambapo 2015 atakuwa Rais.



Akizungumzia kuhusu mchakato wa katiba, Jussa alisema hawatakubali rasimu ambayo haitazingatia matakwa ya Wazanzibari ambayo ni muundo wa serikali tatu ili bendera ya Zanzibar ipepee katika Umoja wa Mataifa (UN).



Pia alisema suala la uraia na uhamiaji Zanzibar ni muhimu kwani ni kisiwa hivyo lazima kuwe na udhibiti wa wageni kutoka nje ya Zanzibar na kila Mzanzibari kuwa na paspoti ya nchi hiyo.



ALIVYOFUKUZWA

Agosti 16, mwaka jana Himid alivuliwa uanachama wake na Kamati Kuu Maalum ya Zanzibar iliyokaa chini ya Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Ali Mohamed Shein..



Agosti 26, mwaka jana Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ikikutana mjini Dodoma iliridhia maamuzi ya Kamati Kuu maalum ya Zanzibar ya kumvua  uanachama baada ya kusikiliza na kuridhia tuhuma dhidi yake kama zilivyokuwa zimekwisha kuamulia Zanzibar.



TUHUMA MAHUSUSI

Katibu wa NEC Itikadi na Unezi wa CCM, Nape Nnauye alidai Himid alishindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.



Nape alitaja tuhuma nyingine ni kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM.



Tuhuma nyingine ni kuikana Ilani ya CCM ya uchaguzi Mkuu wa CCM wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.



MANSOUR NI NANI HASA

Mansour aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Rais Karume mwaka 2000 na kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri wa Maji, Nishati Ujenzi na Ardhi hadi mwaka 2005.



Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki kupitia CCM, nafasi ambayo amedumu nayo hadi sasa. Mwaka huo aliteuliwa na Rais Karume kuwa Waziri wa Maji, Nishati Ujenzi na Ardhi hadi mwaka 2010.



Kati ya 2005 -2010 alikuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar  wadhifa ulimpa fursa ya kuwa Mjumbe wa NEC na Kamati Kuu ya CCM. Mwaka 2010 hadi mwaka 2012, alikuwa Waziri wa Kilimo na Rasilimali.



Ilipofika 2009 alikuwa mstari wa mbele kuushutumu Muungano kuwa ni chanzo cha kudorora kwa Zanzibar huku akiendesha kampeni juu ya suala la mafuta kutokuwa la Muungano.

Katika uchaguzi wa mwaka jana ndani ya CCM, Mansour hakugombea nafasi yoyote ndani ya CCM.



Aidha, alihudumu kama mjumbe wa Baraza la Biashara la Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi 2012.



Kutokana na misimamo yake ndani na nje ya chama na Serikali, Oktoba 15, 2012, Dk. Shein ilifuta uteuzi wa Mansour kama waziri hivyo kubakia kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi hadi alipofukuzwa mwaka jana.



Mansour ni mwanasiasa na mfanyabiashara aliyezaliwa Novemba 3, 1967 kisiwani Unguja. Alisoma masomo yake ya msingi na sekondari nchini India kati ya mwaka 1976 na 1987.



Kabla ya kuingia rasmi katika siasa mwaka 2000, aliteuliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi na alijihusisha katika biashara ya hoteli.



Mwanasiasa huyo ni mtoto wa Mkuu wa Kwanza wa Jeshi la Zanzibar baada ya Mapinduzi, Brigedia Jenerali Yussuf Himid.



Amekuwa akisimamia maridhiano ya Wazanzibari na Umoja wa Kitaifa akiwa mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano aliyoshiriki kikamilifu kuyaanzisha mwaka 2009.



Pia ni miongoni mwa Wazanzibari walio mstari wa mbele kutetea muundo wa Muungano, utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment