Siku moja baada ya mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu na kusababisha kifo na kujeruhi watu saba eneo la Darajani mjini Unguja, mmoja wa majeruhi ameelezea jinsi mwenzao alivyouawa wakati wakisubiri daladala baada ya kutoka kuswali msikitini.Shuhuda huyo, Khalid Ahmed amesema mwenzao alipigwa kwa kitu kinachosadikiwa ni bomu kilichorushwa na kutua mwilini na kufa papo hapo huku wengine wakijeruhiwa.Tukio hilo limethibitishwa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna Yussuf Ilembo na kumtaja marehemu kuwa ni Muhammad Khatib Mkombalaguha (26), Msambaa na mkazi wa Tanga ambaye alikufa papo hapo.
Aidha, kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limewatangazia hali ya hatari wahusika, huku uchunguzi ukianzia kwenye mabaki ya vitu vilivyokutwa katika eneo la tukio.
Akielezea tukio hilo, Ilembo alisema mtu aliyekufa na wengine waliojeruhiwa, walikuwa wametoka Msikiti wa Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia saa 1:45 usiku na kuendelea, lakini huishia kabla ya swala ya alfajiri. Mbali ya Ibada, pia walitoa mawaidha msikitini.
Alisema mara baada ya kumaliza ibada hiyo walitoka msikitini na kufika eneo la Darajani wakisubiri gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao unasadikiwa kuwa ni bomu na kuwajeruhi saba na wanane kufa papo hapo.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo ambalo limezusha taharuki kubwa kwa wananchi wa Zanzibar katika kipindi hiki kumekuwepo na ugeni wa watu mbalimbali,” alisema.
Katika hatua za kwanza za upelelezi, Ilembo alisema wamekusanya baadhi ya vielelezo ikiwemo vipande vya mabaki ya gundi ya karatasi (solar tape) na vitu vingine ambavyo vinasadikiwa vimetumika kwa ajili ya kutengeneza bomu hilo.
Pia katika mlipuko huo, magari mawili, moja aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili Z 675 na jingine aina ya Toyota IST lenye namba za usajili Z 268 yaliharibiwa kwa kuvunjwa vioo na matairi yake kupasuka.
Katika ajali hiyo waliojeruhiwa na kulazwa katika hospitali ni Hamad Nassor Kassim (46), ambaye ameumia kichwa, Khalid Ahmed Haidar (16), Ahmed Haidar Jabir Alfarsy (47) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Al-Rahma. Wengine ni Suleiman Ali Juma (21) amelazwa katika Hospitali ya Al-Rahma huku Kassim Issa Muhammad akiruhusiwa baada ya kupata matibabu.
Naye Ahmed ambaye ni mmoja ya mashuhuda wa ajali hiyo, alisema kitu hicho kinachosadikiwa kuwa ni bomu kilirushwa kwa mkono na kumpata moja kwa moja Mkombalaguha na baadaye kuwajeruhi watu wengine.
“Bomu lile linaonekana moja kwa moja kuwa ni la kurushwa kwa mkono kwa sababu lilimfikia mwilini marehemu na baadaye kutuathiri wengine,” alisema.
Mji wa Zanzibar wiki hii umekuwa na ugeni mkubwa kutoka nchi mbali mbali za Afrika ya Mashariki wakihudhuria ibada ya Kiislamu ya Ijitimai inayofanyika huko Fuoni.
Aidha, wageni mbalimbali wanahudhuria Tamasha la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF) ambalo huwakutanisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi zaidi katika eneo la Darajani lenye mkusanyiko mkubwa wa watu pamoja na kuweka vizuizi katika baadhi ya barabara zinazotoka vijijini kuingia mjini
No comments:
Post a Comment