Amina anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa
tuhuma hizo na amefunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014.
Akisimulia masahibu yaliyompata akiwa katika Wodi Namba Tatu
ya hospitali hiyo, Yusta alisema: “Nililetwa Dar es Salaam mwaka 2010 kufanya
kazi za nyumbani baada ya bosi wangu (Amina) ambaye ni binamu yangu kuzungumza
na mama yangu na kuniomba nije kumsaidia kazi ndogondogo.”Mfanyakazi wa ndani,
Yusta Lucas (20) amekumbana na masahibu yanayofanana na yale ya mtoto Nasra
Mvungi (4) aliyekuwa amefungiwa kwenye boksi kwa miaka karibu minne huko
Morogoro. Huyu amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam
akiuguza majeraha yanayotokana na kuteswa na kufungiwa ndani kwa miaka mitatu.
Binti huyo, mwenyeji wa Mkoa wa Tabora, katika Kijiji cha
Kampala amedai kuwa amekuwa akiteswa na kufungiwa ndani ya nyumba na tajiri
yake, Amina Maige wa Mwananyamala, Kwa Manjunju katika kipindi chote
hicho.Alisema aliishi vizuri na mwajiri wake huyo, lakini mwaka 2012 ndipo
mambo yalipoanza kubadilika akidai kuwa Amina alianza kumwadhibu kwa kumng’ata
na kumchoma kwa pasi kila alipomtuhumu kutokufanya kazi zake vizuri.
“Alikuwa akinichapa na kuning’ata sehemu mbalimbali wakati
mwingine usoni, pia kunichoma kwa pasi yenye moto kila aliponituhumu
kutokufagia au kupiga deki vizuri.”
Hakuwahi kupelekwa hospitali
Alisema licha ya kupata vidonda kutokana na adhabu hizo,
mwajiri wake huyo hakuwahi kumpeleka hospitali na pale alipoona hali ni mbaya
alimnunulia dawa… “Tunaishi wawili tu baada ya kuondoka mumewe na mtoto wake
kumpeleka shule ya bweni… niliugulia hadi nikapona bila mtu mwingine kufahamu.”
“Akienda kazini anafunga geti na kunikataza kufungua hata
kama mtu atagonga… sokoni nilikuwa naenda siku ambazo yeye yupo tu na huwa
akiniamrisha niende haraka na kurudi pasipo kuzungumza na mtu yeyote.”
Alisema mwajiri wake huyo alikuwa akituma pesa za mshahara
wake kwa mama yake akisema ndiye anayepaswa kulipwa, jambo ambalo anadhani
limemfanya mama yake kuhisi mwanaye yuko katika mikono salama… “Kila alipotuma
alipiga simu na kunipa niongee na mama kuhakikisha kama zimefika huku
akinisimamia na baada ya hapo anachukua simu.”
Ataka kurudi kwao
Binti huyo ambaye sehemu kubwa ya mwili wake ina alama za
kung’atwa meno na majeraha ya kuchomwa na pasi, alisema: “Ninaomba mtu yeyote
mwenye hela, nataka nikitoka hapa hospitali nirudi Tabora kwa mama. Nina shaka
na maisha yangu hapa kwa huyu mama… sitaki tena kubaki Dar es Salaam kutokana
na mateso ninayoyapata.”
Polisi wasema
Mkaguzi Msaidizi wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Prisca Komba alisema taarifa za binti huyo ziliwafikia baada ya
majirani kupeleka taarifa hizo katika Kikundi cha Kipange kilichopo Kwa
Manjunju ambacho nacho kilitoa taarifa polisi na ndipo mtego wa kumnasa
mwanamke huyo ukawekwa.
Majirani walichukua hatua hiyo kutokana na kusikia kelele za
kilio mara kwa mara zikitokea ndani ya nyumba ya mtuhumiwa. “Tumekagua makovu
na majeraha mbalimbali yaliyo katika mwili wake na kupata jumla kuwa yako 91,”
alisema Komba na kuongeza:
“Toka jana amekuwa akinitaka nisiondoke mbali naye amekuwa
na hofu, lakini sasa afadhali kidogo baada ya kumpatia ushauri na kumhakikishia
kwamba hapa yuko salama.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Thobias Edoyeka alisema
suala hilo linashughulikiwa na polisi pamoja na ustawi wa jamii, kauli
iliyoungwa mkono na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mwananyamala, Rose Temu ambaye
alisema wanafuatilia kwa karibu matibabu yake pamoja na usalama wake. “Hali
yake ikishaimarika na kujiridhisha kuwa anaendelea vizuri, tutakuwa na jukumu
la kumuunganisha na familia yake,” alisema.
Ofisa Muuguzi Msaidizi Wodi Namba Tatu ambayo ni ya
kinamama, Rose Mussa alisema Yusta anaendelea vizuri.
“Anaendelea vizuri kwa kweli, jana (juzi) hakuwa hivi alikuwa
mwoga hawezi kujieleza tofauti na leo (jana)… bado anaendelea na vipimo,
tutakapoona anafaa kuruhusiwa tutafanya hivyo na kumkabidhi kwa ustawi wa
jamii.”
Credit: Mwananchi
No comments:
Post a Comment