Shirikisho la FIFA linataka uchunguzi uwe wazi
Wachezaji wa Cameroon wakichapana katika mechi yao uwanjani
Maafisa wa Cameroon watapelelezwa kutokana na madai kwamba
saba kati ya wachezaji wa timu ya taifa hilo walihusika katika kupanga mechi
katika Kombe la Dunia linaloendelea nchini Brazil.
Kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda la taifa hilo
litachunguza shutuma za "udanganyifu" wa "wachezaji saba
wabaya" katika mechi zao tatu za makundi.
Madai hayo yametolewa na gazeti moja la kijerumani na mtu
aliyehukumiwa kwa kuhusika na kupanga mechi nchini Singapore.
Cameroon ilipoteza mechi zote za kundi A, ikiwemo ile
waliolazwa na Croatia kwa mabao 4-0.
Mchezaji wa 'The Indomitable Lions' Alex Song, alionyeshwa
kadi nyekundu kwa kumgota Mario Mandzukic mgongoni katika mechi hiyo, huku
wachezaji wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakizozana baadaye
katika mechi hiyo.
Ripoti kutoka katika shirikisho la kandanda la Cameroon
lilisema: "Madai yaliyotolewa majuzi kuhusu udanganyifu katika mechi tatu
za mwanzo za Cameroon katika Kombe la Dunia la 2014, hasa kati ya Cameroon na
Croatia, na vile vile 'kuwepo na wacheza saba wabaya katika timu yetu ya taifa'
hayaambatani na maadili na kanuni zinazopendekezwa na usimamizi wetu, pamoja na
kanuni za Fifa na maadili ya taifa letu.
"Tuna nia kuu ya kutumia mbinu zote zinazostahili ili
kutatua swala hili linalosumbua kwa muda mfupi iwezekanavyo."
'FIFA yataka uchunguzi wa wazi'
Fifa haikusema iwapo ilikuwa ikichunguza swala hilo au la,
kwani bodi hiyo inayosimamia kandanda ulimwenguni "ilitaka uchunguzi uwe
wazi".
Hata hivyo, iliongezea kuwa: "kwa ujumla, uadilifu
katika mchezo huu ndio swala linalopewa kipaumbele na Fifa, kwa hivyo,
tunatilia madai yoyote kuhusu udanganyifu maanani sana."
'Mgogoro wa marupurupu'
Matayarisho ya Cameroon kabla ya michezo hiyo nchini Brazil
yalitatizika baada ya wachezaji kukataa kupanda ndege kuelekea Brazil hadi
wakati mgogoro uliohusiana na wachezaji hao kulipwa marupurupu yao
ulipotatuliwa.
Maelewano ya fedha hatimaye yalifikiwa na shirikisho la
kandanda la Cameroon, Fecafoot, lakini safari ya kikosi hicho kuelekea Brazil
ilikuwa imecheleweshwa kwa takriban siku nzima.
Walianza michezo hiyo kwa kushindwa kwa bao 1-0 na Mexico
kabla ya kulazwa na Croatia na wenyeji Brazil waliowafunga mabao 4-1.
"Wachezaji kadhaa walikosa nidhamu, na ndio sababu
tumefungwa mabao manne," mkufunzi wa Cameroon Volker Finke aliambia gazeti
la kifaransa la L'Equipe baada ya kushindwa na Croatia.
"Ninajua ni vigumu kucheza na wachezaji kumi, lakini
hilo si sababu ya kupoteza katika mkondo huu.
"Mechi ilikuwa sawa hadi tulipoonyeshwa kadi nyekundu.
Wacroatia walifanya vizuri mbele ya lango lakini Cameroon pia ilikuwa na nafasi
ya kufunga.
"Tabia ya wachezaji kadhaa kwa kweli sio nzuri. Hata
tulipokuwa bado na wachezaji 11 kila upande, haikuwa ya kupendeza.",(A.I)
No comments:
Post a Comment