Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, July 31, 2014

DK.KITILLA AFICHUA SIRI YA ZITTO KWENDA MAHAKAMANI


MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo, amefichua siri ya kwenda mahakamani kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), kwamba ni baada ya jopo la wasomi kumshauri kufanya hivyo.

Dk. Kitilla alisema kabla ya hapo, mbunge huyo 

alikuwa tayari kuwaachia viongozi wa chama chake wamvue uanachama kama alivyofanyiwa yeye na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati akiendesha mafunzo ya siku moja kwa viongozi wa mikoa na wajumbe wa Chama cha ACT–Tanzania juu ya historia, misingi, itikadi na falsafa ya chama hicho.

Alisema kwamba jopo la wasomi walimuelezea Zitto umuhimu wa kuangalia maslahi ya watu waliomchagua na njia inayotaka kutumika kufikia uamuzi wa kumvua uanachama wake katika chama hicho.

“Sisi tuliridhia kuvuliwa uanachama kwa kuwa hakukuwa na maslahi ya moja kwa moja yanayoweza kuathiri maisha yetu na familia zetu, lakini kwa Zitto hilo lingetokea na kumuathiri kwa mazingira yote mawili,” alisema.

Kuhusu kuandaa waraka unaodaiwa kuwa ni wa usaliti ndani ya CHADEMA, Dk. Kitilla alisema katika utatu wao wakiwa wanachama wa CHADEMA wakati huo walikuwa na nia ya mabadiliko ya muda mrefu ndani ya chama hicho baada ya kubaini baadhi ya mambo hayaendi sawa.

“Mimi, Mwigamba na Zitto tumekuwa na nia ya muda mrefu ya kuleta mabadiliko ndani ya CHADEMA, matamanio yetu ya mabadiliko yalihitimishwa kwa kuandika waraka wa mabadiliko, ukiainisha sababu za mabadiliko na mikakati yetu ya kushinda uchaguzi ndani ya chama,” alisema Dk. Kitilla.

Aliongeza baada ya Mwigamba kukutwa na waraka wa mabadiliko uliodhaniwa kuwa ni uhaini, walifukuzwa ndani ya chama hicho na kwamba hawakuona sababu ya kujiunga na chama kingine chochote cha siasa katika vyama vilivyopo.

Kwamba baada ya hali hiyo, vyama mbalimbali viliwafuata na kutaka wajiunge navyo, ikiwamo CCM, na waliwakatalia kwa kuamini kujiunga na chama hicho ni usaliti wa dhamira zao katika kufikia mabadiliko, na kuwa nchi ilipofika sio muda wa kukisaidia kuendelea kubaki madarakani.

Alisema matatizo yaliyopo katika vyama vya upinzani ni ya asili na yanafanana kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa umakini, kuwepo kwa hisia umiliki pamoja na kukosekana kwa demokrasia.

Dk. Kitilla ambaye kwa sasa ni mshauri wa ACT-Tanzania, alisema iwe ni marufuku kwa mwanachama wa chama hicho kuzungumzia vyama vingine badala ya kuwazungumzia wananchi na matatizo yao.

Chanzo:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment