Pages

Wednesday, July 23, 2014

Kikao cha CCM, UKAWA chavunjika




    KIKAO kati ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimeshindwa kupata muafaka baada ya pande hizo mbili kuendelea kuvutana hadi jana jioni.Kikao hicho cha siri kilichoanza jana saa nne asubuhi katika Hoteli ya Sea cliff iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, kiliongozwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Fransis Mutungi.
Jaji Mutungi aliingilia kati suala hilo, baada ya kuona muafaka wa Ukawa kurudi bungeni umekwama kutokana na madai ya wajumbe wa 

CCM wanajadili mambo yasiyokuwamo ndani ya rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
Madai mengine ya Ukawa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kutumia madaraka yake vibaya ikiwa ni pamoja na kupindisha kanuni za Bunge hilo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mutungi alilazimika kuwaita viongozi wa CCM na Ukawa ili waweze kuwapatanisha ikiwa ni pamoja na kuwataka Ukawa warudi bungeni katika kikao kijacho ambacho kinatarajiwa kuanza Agosti 5, mwaka huu.
  Ukawa unaundwa na vyama vitatu vya Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha NCCR-Mageuzi.
Akizungumza na MTANZANIA kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, alisema mpaka jana jioni hakuna muafaka katika kikao hicho kutokana na kuendelea kuvutana.
 “Nimetoka kwenye kikao lakini hakuna muafaka, hii inatokana na pande mbili kuendelea kuvutana, kwa hiyo nimewaacha waendelee kujadili suala hilo,” alisema Lissu. Alisema msajili ndiye aliyeitisha kikao hicho ikiwa ni pamoja na kutafuta muafaka wa suala hilo, lakini kwa dalili zinazoonekana hakuna muafaka hapo. Hivi karibuni, Ukawa walidai kuwa hawawezi kurudi tena kwenye Bunge hilo mpaka wajumbe hao wa CCM watakapokubali kujadili rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Warioba.Kumekuwa na juhudi mbalimbali za kutafuta muafaka kuhusu suala hilo ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, taasisi za kiraia na wadau mbalimbali ambao kwa pamoja wamekuwa wakiwasihi Ukawa warudi bungeni ili kujadili rasimu hiyo.
  Source: Mtanzania

No comments:

Post a Comment